Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dk.Stergomena Tax akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukutana na wadau wa maendeleo wakiwemo Mabalozi na Wakuu wa taasisi za kimataifa leo Januari 30,2023 jijini Dodoma.
…………………………….
Na Alex Sonna-DODOMA
SERIKALI imekutana na wadau wa maendeleo wakiwemo Mabalozi na Wakuu wa taasisi za kimataifa huku ikiwahakikishia watanzania na wadau hao kuwa nchi ipo salama na hakuna matishio yoyote ya kiusalama.
Hayo yamesema leo Januari 30,2023 jijini Dodoma na Waziri wa Mambo ya Nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki Dk.Stergomena Tax,wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukutana na wadau hao .
Kauli ya serikali inafuatia baada ya uwepo wa uvumi kuwa kuna matishio ya kiusalama na vurugu ndani ya nchi hali iliyopelekea Shirika la ndege la Uholanzi (KLM),kusitisha safari zake nchini.
“Wiki iliyopita kulikuwepo na uvumi kuwa kuna matishio ya vurugu ndani ya nchi yetu hadi Shirika la ndege la KLM, kusitisha safari zake nchini, serikali ilianza kuzifanyia kazi na Polisi walitoa taarifa pia Waziri Ujenzi na Uchukuzi Makame Mbarawa, alitoa taarifa kuwa anga letu ni salama.
“Kutokana hali hiyo tumewaita wadau wa maendeleo wakiwemo mabalozi na kuwahakikishia kuwa hali yetu ni salama kabisa hakuna tishio lolote la kiusalama tunawahakikishia Watanzania na Dunia kwa ujumla kuwa Tanzania ni salama na tuwashukuru wale wote hata uwepo wa taarifa hizo waliendelea kuja nchini”amesema Dk.Tax
Aidha amesema kuwa katika kikao hicho na wadau hao wamekubaliana kuwa hali hiyo haitajitokeza tena na wataendelea kufanya kazi kwa kushirikiana.
”Nchi inathamini mchango wao na inawathamini kama wadau wa maendeleo na wapo tayari kufanya nao kazi katika maeneo yote ikiwemo amani na usalama.”amesema Dk.Tax