Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma ametoa rai kwa Wadau wa Mhimili huo na wananchi walioshiriki na kutembelea maonesho ya Wiki ya Sheria kuwa chachu ya kuhamasisha usuluhishi dhidi ya migogoro mbalimbali inayojitokeza katika jamii ili kulinda amani na kukuza uchumi.
Akizungumza na Watumishi wa Mahakama, Wadau na Wananchi walioshiriki katika hafla ya kufunga Maonesho ya Wiki ya utoaji elimu ya Sheria katika Viwanja vya Nyerere ‘Square’ leo tarehe 29 Januari, 2023, Mhe. Chuma amesema kuwa, kwa kufanya hivyo watakuwa wanatekeleza kwa vitendo Kaulimbiu ya wiki ya sheria ya mwaka huu isemayo; “Umuhimu wa Utatuzi wa Migogoro kwa Njia ya Usuluhishi katika Kukuza Uchumi Endelevu: Wajibu wa Mahakama na Wadau.”
“Ni imani yangu kwamba kila Taasisi iliyoshiriki maonesho haya imejipambanua ipasavyo kwenye kauli mbiu hii, kuelimisha wananchi na kuonesha utayari wao wa kusaidia utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi kwa maslahi mapana ya kusaidia wananchi kukuza uchumi wao na wa nchi yetu kwa ujumla,” amesema Mhe. Chuma.
Mahakama katika utaratibu wake wa kuelimisha umma itaendelea kuhimiza na kuuelimisha juu ya faida za utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi. “Kimsingi, usuluhishi ni takwa la kikatiba na ni kwa mujibu wa ibara ya 107A (2) (d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesisitiza Msajili Mkuu.
Mhe. Chuma ameainisha faida za usuluhishi ambazo ni pamoja na kupunguza mlundikano wa mashauri mahakamani, kupunguza gharama na kujenga au kulinda amani na kuongeza kuwa, usuluhishi ni agizo la maandiko matakatifu huku akitoa mifano wa Waebrania 12:14 inaelekezwa kuwa tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, Mathayo 5:9 inaainisha kuwa heri wapatanishi; maana hao wataitwa wana wa Mungu. Nayo, Mathayo 5:25-26 inaelekeza kuwa njooni upatane na mshtaki wako wakati unaenda naye kortini, asije mshtaki wako akakukabidhi kwa hakimu, na mwamuzi kwa walinzi au kufungwa gerezani.
Aidha; Msajili Mkuu ameonesha kuridhishwa na idadi ya Taasisi/Wadau walioshiriki katika Maonesho hayo, ambayo idadi yao ni Taasisi 38 zilizoshiriki katika maonesho hayo na kueleza kuwa mwitikio huo unatokana na mahusiano mazuri ya Mahakama na wadau na utayari wa wadau kushirikiana na Mahakama kwa kutoa mchango wao katika kuelimisha wananchi na kuboresha huduma za upatikanaji haki.
Aliongeza kuwa, anaamini kwamba, ushirikiano huu utasaidia kuimarisha mahusiano na mazingira mazuri ya utoaji haki na utoaji huduma kwa ujumla kwa wananchi wanaowahudumia. Vilevile amewaomba Wadau kutenga bajeti za kutosha kwa ajili ya kuweka mazingira wezeshi katika matumizi ya TEHAMA kwa lengo la kuendelea na kasi ya karne ya 21.
Kadhalika, Mhe. Chuma amewashukuru Viongozi waliopata nafasi ya kushiriki na kutembelea maonesho ya Wiki ya Sheria yaliyofanyika kitaifa jijini Dodoma, Viongozi hao ni pamoja na; Mhe. Dkt. Philip Isidor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Damasi Ndumbaro (Mbunge) Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Rosemary Senyamule, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Salma Maghimbi, Jaji wa Mahakama Kuu na Mwenyekiti wa Baraza la Ushindani, Prof. Elisante ole Gabriel Mtendaji Mkuu wa Mahakama na wengine.
Mbali na Wadau, Msajili Mkuu amevishukuru pia Vyombo vya Habari kwa kazi nzuri waliyofanya ya kuuhabarisha umma katika kipindi chote cha maonesho na kuwaomba kuendelea kutoa taarifa sahihi za Mhimili huo zinazozingatia usawa wa pande zote muhimu za taarifa husika.
Wiki ya Sheria nchini ilizinduliwa rasmi tarehe 22 Januari, 2023 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango ambaye alizindua kwa ngazi ya kitaifa. Aidha, kilele cha Siku ya Sheria nchini kwa mwaka huu itakuwa tarehe 01 Februari, 2023 ambapo kitaifa itafanyikia katika Viwanja vya Chinangali mkoani Dodoma na Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Miongoni mwa Wadau walioshiriki katika Maonesho hayo ni pamoja na Chama Cha Wanasheria Wanawake (TAWLA), Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Tume ya Haki za Binadamu, Tume ya Kurekebisha Sheria, Tume ya Utumishi ya Mahakama, Taasisi ya Usuluhishi, Baraza la Ushindani, Ofisi ya Mkemia Mkuu Wa Serikali, Mamlaka ya Kuthibiti Dawa za Kulevya, Kamisheni ya Usuluhishi na Uamuzi, Kituo cha Haki za Binadamu, OSHA.
Wengine ni Taasisi ya Mafunzo ya Sheria kwa Vitendo (LST), RITA, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wizara ya Katiba na Sheria, NMB, TAKUKURU, Wakili Mkuu Wa Serikali, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Chama Cha Majaji Wanawake (TAWJA), Mahakama ya Afrika Mashariki, Jeshi la Magereza, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Chuo Cha uongozi wa Mahakama Lushoto, Idara ya Uhamiaji, Wizara ya Ardhi Nyumba Na Maendeleo ya Makazi, Jeshi la Zimamoto, Jeshi La Polisi, Tume ya Taifa ya Uchaguzi, BRELA na wengine.
Sehemu ya Watumishi wa Mahakama pamoja na Wadau wakisikiliza hotuba ya kufunga Maonesho ya Wiki ya Sheria iliyokuwa ikitolewa na Mgeni Rasmi Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma (hayupo katika picha) wakati wa hafla ya kufunga Maonesho hayo katika Viwanja vya Nyerere ‘Square’ jijini Dodoma.
Kwaya ya Mahakama ikitumbuiza katika hafla ya kufunga Maonesho ya Wiki ya Utoaji elimu ya Sheria.
Meza kuu wakiwafuatilia wanakwaya (hawapo katika picha) walipokuwa wakitoa burudani wakati wa tukio la kufunga Maonesho ya Wiki ya Utoaji Elimu ya Sheria. Katikati ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma, wa pili kushoto ni Msajili wa Mahakama ya Rufani na Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Wiki na Siku ya Sheria, Mhe. Sylivester Kainda, wa pili kulia ni Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt, wa kwanza kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani (T) na Katibu wa Kamati ya Maandalizi ya Wiki na Siku ya Sheria, Mhe. Charles Magesa na wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Maboresho (JDU), Mhe. Dkt. Angelo Rumisha.