******************
Na Rayson, WAF – Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Afya imebainisha mikakati itayosaidia katika kutokomeza ugonjwa wa ukoma nchini ifikapo mwaka 2030, ikiwemo kutoa mafunzo elekezi kwa watoa huduma hasa katika maeneo ambayo ugonjwa wa Ukoma bado ni tatizo kubwa na kuongeza elimu kwa jamii juu ya ugonjwa huo.
Mikakati hiyo imebainishwa leo Januari 29, 2023 Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel wakati akisoma tamko kwa niaba ya Waziri wa Afya katika kuelekea kilele cha siku ya Ukoma Duniani chenye kauli mbiu ya “Chukua hatua sasa, tokomeza Ukoma nchini.”
“Serikali yetu imeendelea kuchukua hatua muhimu ili kufikia malengo ya utokomezaji wa Ukoma katika Taifa letu na tayari tumetengeneza mkakati wa kufikia visa sifuri vya Ukoma ifikapo mwaka 2030 ikiwemo mkakati wa kutoa mafunzo elekezi kwa watoa huduma hasa katika maeneo ambayo Ukoma bado ni tatizo kubwa.” Amesema Dkt. Mollel.
Ameendelea kusema kuwa, kupitia Wataalamu katika maeneo ya kutoa huduma za Ukoma, Wizara imelenga kufanya uchunguzi wa Ukoma katika kaya zote zenye wagonjwa ili kuwabaini na kuwaanzishia huduma mara moja kwa wataogundulika.
Pia, Dkt. Mollel amesema, Wizara imelenga kuongeza uwezo wa ufuatiliaji wa mwenendo wa ugonjwa wa Ukoma katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchini ili kuimarisha mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
Sambamba na hilo Dkt. Mollel amesema, Wizara inaendelea na juhudi za kufanya tafiti na kuibua mbinu bunifu za kuharakisha kasi ya utokomezaji wa ugonjwa huo inaongezeka kwa kutambua mbinu mbalimbali za mapambano dhidi ya magonjwa huo.
Mbali na hayo, Dkt. Mollel amewaelekeza Waganga Wakuu wa Halmashauri kuhakikisha wanajumuisha shughuli za kutokomeza ugonjwa wa Ukoma katika mikakati mingine ya afya katika Halmashauri zao.
Mikoa na Halmashauri kuhakikisha kila mgonjwa anayeibuliwa anatambuliwa makazi yake, Kijjiji, Kata atokako, iwe ndani ya wilaya husika au nje ya mkoa, huku akisisitiza iwapo mgonjwa atatokea nje ya Mkoa, ihakikishwe taarifa zake zinapelekwa alikotokea ili kufanya ufuatiliaji na kuiifanyia uchunguzi wa Ukoma na kuipatia tibakinga kaya husika.
Aliendelea kusisitiza kuwa, kila Halmashauri kuhakikisha wanafuatilia mwenendo wa ugonjwa wa Ukoma na wanakuwa na takwimu sahihi za wagonjwa kulingana na maeneo au vijiji au mitaa wanakopatikana wagonjwa hao.
Aidha, Dkt. Mollel amewahakikishia kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan itaendelea kuhakikisha zinapatikana dawa za kutosha nchini kote na wagonjwa wote wanatibiwa bure.