Jaji mfawidhi wa Mahakama Kuu kanda ya Songea Dkt Yose Mlyambina katikati,Jaji wa Mahakama kuu kanda ya Songea Upendo Madeha wa tatu kushoto, wakiwa katika picha ya pamoja na wadau waliofanikisha bonanza la michezo mbalimbali lililoandaliwa na mahakama katika wiki ya sheria nchini.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu kanda ya Songea Dkt Yose Mlyambina akizungumza kabla ya kufunga bonanza la michezo katika uwanja wa shule ya msingi Sokoine Manispaa ya Songea,kulia kwake Jaji wa Mahakama Kuu kanda ya Songea Upendo Madeha.
*******************************
Na Muhidin Amri,
Songea
JAJI Mfawidhi wa Mahakama Kuuu kanda ya Songea Dkt Yose Mlyambina,amewaongoza watumishi wa mahakama,taasisi na idara za serikali katika bonanza la michezo mbalimbali likiwa na lengo la kuboresha afya ,kujikinga na magonjwa,kuleta mahusiano na kufahamiana.
Akizungumza kabla ya kufunga Bonanza hilo lililofanyika katika uwanja wa shule ya msingi Sokoine Manispaa ya Songea Jaji Dkt Mlyambina,amewahimiza vijana mkoani Ruvuma kutumia muda wao kufanya mazoezi na kushiriki katika michezo mbalimbali ili kujiweka sawa kiafya,kiakili badala ya kutumia muda wao kwenye ulevi.
Alisema,bonanza hilo limekuwa na faida nyingi ikiwamo kuboresha afya, kuimarisha mahusiano kati ya watumishi na wadau wa mahakama na taasisi nyingine za serikali,kufahamiana na kuondoa ukuta(wigo)kati ya mahakama na wananchi.
Alisema,mtu anayefanya mazoezi kwa kawaida anakuwa na afya ya akili,ana imarisha mwili na kuongeza siku za kuishi na kuwaasa wananchi wa mkoa huo ,kuwa na utaratibu wa kushiriki katika michezo na mabonza mbalimbali ili kulinda afya zao.
Aidha Jaji Dkt Mlyambina alisema,katika maadhimisho ya wiki ya sheria watumishi wa mahakama wametoa elimu ya sheria kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari,sokoni,na wananchi waliofika kwenye mabanda ya maonyesho katika viwanja vya soko kuu Songea.
Wiki ya Sheria mwaka huu ilifunguliwa tarehe 22 mwezi huu na imefungwa leo (jana) tarehe 29 Januari chini ya‘Kauli mbiu umuhimu wa utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi katika kukuza uchumi endelevu na wajibu wa mahakama na wadau’.
Kwa upande wake mdau wa michezo meneja wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma Ephatar Mlavi,ameipongeza mahakama kanda ya Songea kuandaa bonanza hilo kwani limesaidia kukutanisha wadau mbalimbali,watumishi wa idara na taasisi za serikali na wananchi.
Alisema,bonanza hilo limekuwa na mafanikio makubwa kwani limewezesha washiriki kupata nafasi ya kufanya mazoezi na kuboresha afya zao na kushauri liendelee kufanyika mwaka hadi mwaka.
Awali mratibu wa bonanza hilo wakili Abel Ngilangwa,alitaja michezo iliyochezwa ni mpira wa miguu kwa wanaume,mpira wa pete,kufukuza kuku,kukimbia kwenye magunia mbio za mita 100 na 200,kuvuta kamba,kukimbia na yai kwenye kijiko na kukimbiza kuku.
Ngilangwa alieleza kuwa,lengo kuu la bonanza hilo ni kutoa elimu ya sheria,kuimarisha mahusiano kati ya Mahakama na wananchi,kuimarisha afya za watumishi kupitia michezo ili kuondoa magonjwa yasiyoambukiza.
Alisema,michezo hiyo ni kielelezo halisi kinacho thibitisha jamii umoja na ushirikiano ndani ya mahakama katika kuhakikisha lengo la mahakama kuu Tanzania kuifikia jamii na ni chombo kinachofikika kwa urahisi.