**************************
NA MWAMVUA MWINYI, BAGAMOYO
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) kitengo cha forodha Wilaya ya Bagamoyo kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya kupitia Idara ya Afya, Usafi wa mazingira na Udhibiti wa taka ngumu, imeteketeza bidhaa zilizoingizwa kwa njia ya magendo zenye thamani ya sh. milioni 25.
Akizungumza wakati wa uteketezaji huo ,katika dampo la Sanzale lililopo Kata ya Magomeni ,Ofisa Mwandamizi wa Forodha Bagamoyo Noel Makere alisema bidhaa hizo zilikamatwa katika doria zinayofanywa na ofisi hiyo.
Alitaja bdhaa hizo ni pamoja na betri dazeni 12, matairi ya magari na pikipiki yaliyotumika (Used Tyres) 400, Nguo za mitumba balo 9 na vilainishi ‘lubricants’ lita 960.
Bidhaa nyingine ni mafuta ya taa lita 300, Friji 2, kompresa za friji 12 na sabuni za unga Kilo 30 .
“Serikali imepiga marufuku bidhaa hizi kuingizwa nchini kwani hazifai kwa matumizi ya binadamu na hazina ubora”
“Matairi haya 400 tunayoteketeza yamekatazwa kabisa kuingizwa na kutumika nchini, bidhaa kama friji na mitumba ni bidhaa zilizozuiwa kuingizwa nchini,”alisema Makere.
Makere alibainisha , bidhaa zote hizo zilizoteketezwa zimethibishwa na shirika la viwango nchini (TBS) kuwa hazifai kwa matumizi ya binadamu.
Alitoa onyo kwa wafanyabishara kuwa wazalendo na kufuata sheria na taratibu za uingizaji bidhaa nchini hususani ulipaji wa kodi ili kuepuka usumbufu na hasara zisizo za lazima.
Nae ofisa Afya wa Wilaya ya Bagamoyo Mohamed Farah aliwaasa ,wafanyabiashara kutii sheria bila shuruti na kuhakikisha bidhaa wanazoingiza kupitia bandari ya Bagamoyo, hazina madhara kwa watumiaji ili kuepuka madhara ya kiafya yanayoweza kusababishwa na matumizi ya bidhaa zilizokosa ubora na zisizofaa kwa matumizi ya binadamu