******************************
Na Mwandishi wetu, Mirerani
MKUU wa Mkoa wa Manyara, Charles Makongoro Nyerere amewataka wadau wa madini ya Tanzanite waipe ushirikiano kampuni ya wazalendo ya Franone Mining & Gem Ltd iliyoshinda zabuni ya kuchimba kwenye kitalu C ili waweze kuchimba ipasavyo.
Makongoro amezungumza hayo mara baada ya kutembelea eneo la kitalu C na kukagua shughuli za uchimbaji wa kampuni hiyo iliyopo mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro.
Amesema kampuni hiyo imeaminiwa na Serikali kuchimba madini ya Tanzanite hivyo wadau wa madini waipe ushirikiano ili ichimbe madini hayo na waadhihirishe kuwa wachimbaji wazawa wanaweza.
“Nawapongeza sana kwa ninyi kushinda zabuni ya uchimbaji wa kitalu C na ninatarajia mtafanikiwa katika uchimbaji wenu bila tatizo lolote sisi wadau wa madini pamoja na Serikali tutawapa ushirikiano mkubwa na wakutosha,” amesema Makongoro.
Hata hivyo, amesema baada ya kampuni ya Franone kutangazwa kushinda zabuni ya uchimbaji kitalu C wanapaswa kuhakikisha eneo hilo lisiwe shamba la bibi kwa mtu kuingia bila ridhaa.
“Suala la kusema machimbo ya kitalu C ni shamba la bibi linapaswa kufikia mwishoni, kwani eneo hilo lilikuwa halitumiki ila hivi sasa mnachimba ninyi Franone,” amesema Makongoro.
Hata hivyo, mkurugenzi wa Flanone, Onesmo Mbise amesema hivi sasa wameziba maeneo yote yaliyokuwa wazi mgodini na kutumiwa kuingia kwenye eneo hilo kwa wizi ili kuiba madini.
“Tumeweka vyuma vinavyopitisha hewa ila mtu hawezi kupita tangu tulivyoshinda zabuni Septemba 15 mwaka 2022 tulijipanga kumaliza changamoto hiyo na tumefanikiwa,” amesema Mbise.
Mkuu wa wilaya ya Simanjiro Dkt Suleima Serera amewapongeza wakurugenzi wa kampuni ya Franone Mining & Gem kwa kushinda zabuni ya kuchimba madini ya Tanzanite.
“Ninyi wakurugenzi watatu ni wazalendo tunatarajia mtafuata kanuni na taratibu za uchimbaji wa madini ikiwemo kutoa ajira na kulipa kodi kwa Serikali na ushuru ya huduma kwa Halmashauri,” amesema Dkt Serera.
Kamanda wa polisi wa mkoa wa Manyara, George Katabazi amesema suala la ulinzi linapaswa kupewa kipaumbele ila kwa sababu mitobozano imeshazibwa wanatarajia hakutakuwa na tatizo.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Simanjiro, Kiria Laizer ameipongeza kampuni hiyo kwa kushinda zabuni hiyo, kwani alishafanya eneo hilo akiwa ofisa rasilimali watu wa kampuni ya TanzaniteOne.
Katibu Tawala wa mkoa wa Manyara, Karolina Mthapula amesema kampuni hiyo ishirikiane na halmashauri ya wilaya ya Simanjiro ili kupangilia kusaidia jamii inayowazunguka.