Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Jones Olotu akizungumza wakati wa kikao maalum cha Waziri wa Nishati, Januari Makamba na Wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini kilichofanyika Dar es Salaam, Januari 24, 2023.
Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Namis Corporate, Mhandisi Thomas Uiso, akizungumza kwa niaba ya Wakandarasi wote wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini wakati wa kikao chao na Mheshimiwa Waziri wa Nishati, Januari Makamba kilichofanyika Dar es Salaam, Januari 24, 2023.
Sehemu ya Wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini wakimsikiliza Waziri wa Nishati, Januari Makamba alipokuwa akizungumza nao katika kikao maalum kujadili utekelezaji wa miradi hiyo. Kikao hicho kilifanyika jijini Dar es Salaam, Januari 24, 2023.
Waziri wa Nishati, Januari Makamba akizungumza na Wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini katika kikao maalum kilichofanyika Dar es Salaam, Januari 24, 2023.
******************************
Veronica Simba – REA
Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umeeleza hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini inayoendelea nchi nzima.
Taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo hadi kufikia sasa, iliwasilishwa na Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi kutoka REA Mhandisi Jones Olotu katika kikao cha Waziri wa Nishati Mheshimiwa Januari Makamba na Wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo kilichofanyika Januari 24 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Akielezea kuhusu Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Kwanza, Mhandisi Olotu alisema umepeleka umeme katika vijiji vyote 3,978 vilivyopo kwenye wigo wa Mradi na kuunganisha wateja wapatao 180,342 kati ya 234,000 sawa na asilimia 77.
Aidha, aliongeza kuwa, kazi ya kuunganisha wateja pamoja na marekebisho madogo inaendelea. “Kwa sasa mradi upo katika kipindi cha uangalizi na gharama za Mradi ni shilingi Trilioni 1.12”
Kuhusu Mradi wa Ujenzi wa Kituo cha Kupoza Umeme cha Ifakara na Ujenzi wa Njia ya Kusambaza Umeme Vijijini katika Wilaya za Kilombero na Ulanga, alisema umelenga kuwezesha uendelezaji na uimarishaji wa shughuli za kilimo cha umwagiliaji katika eneo la SAGCOT (Southern Agriculture Growth Corridor of Tanzania) kwa kuwapatia wananchi huduma za umeme.
Alibainisha kuwa hadi kufikia Disemba 2022, utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa kituo cha kupoozea umeme umefikia asilimia 81.5 na kwamba upande wa mradi wa ujenzi wa miundombinu ya kusambaza umeme umekamilika kwa asilimia 100 katika vijiji 8 na vitongoji 7.
Mkurugenzi Olotu alitaja gharama za Mradi ni shilingi bilioni 23.62 ambazo ni ufadhili wa Umoja wa Ulaya na Serikali ya Tanzania ambapo utekelezaji wake ulianza Machi 2020 na unatarajiwa kukamilika Aprili 2023.
Vilevile, alibainisha kuwa, ujenzi wa miundombinu ya njia za kusambaza umeme kwa wananchi katika vijiji 8 na vitongoji 7 umekamilika kwa asilimia 100 ambapo vijiji vyote vina umeme, wateja wa awali 1,484 kati ya 1,853 wameunganishiwa nishati hiyo.
Mradi mwingine unaotekelezwa ni wa Ujazilizi Fungu la Pili A ambao unalenga kusambaza umeme katika vitongoji 1,318 katika mikoa ya Dodoma, Singida, Shinyanga, Mwanza, Tabora, Kilimanjaro, Mbeya, Pwani na Tanga ili kufikisha umeme katika vitongoji 1,318 na kuunganisha jumla ya wateja wa awali 101,723 kutokana na nyongeza ya maeneo ya kupelekewa umeme.
“Hadi kufikia Disemba 2022, vitongoji 1,103 vimeunganishiwa umeme na wateja 60,074 kati ya 101,723 sawa na asilimia 59 wameunganishwa na huduma za umeme,” alibainisha na kuongeza kuwa gharama ya mradi ni shilingi bilioni 142 ambapo kwa ujumla mradi umefikia asilimia 97 ya utekelezaji na unatarajiwa kukamilika tarehe 30 Aprili 2023.
Kwa upande wa Mradi wa Ujazilizi Fungu la Pili B, alisema unalenga kusambaza umeme katika vitongoji 1,686 ambavyo havijafikiwa na miundombinu ya umeme katika mikoa ya Arusha, Geita, Kagera, Katavi, Kigoma, Lindi, Morogoro, Njombe na Songwe ambapo gharama ya mradi inakadiriwa kuwa shilingi bilioni 227.
Alisema kuwa Mradi unalenga kuunganisha jumla ya wateja wa awali 95,334 ambapo hadi kufikia Disemba 2022, Ununuzi wa Wakandarasi umekamilika na mchakato wa kusaini mikataba unaendelea.
Katika hatua nyingine, Mhandisi Olotu alieleza kuwa Serikali imetangaza zabuni kwa ajili ya kupata wakandarasi watakaotekeleza mradi wa kupeleka umeme katika vitongoji 654 katika mikoa ya Songwe na Kigoma kwa gharama ya shilingi bilioni 100 ikiwa ni mkopo kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF).
Akieleza zaidi, alisema kuwa Mradi huu ni mwanzo wa kutekeleza mpango wa Serikali kufikisha huduma ya umeme katika vitongoji 37,610 nchini ambavyo bado havijafikiwa na huduma za nishati hiyo unaokadiriwa kugharimu kiasi cha shilingi trilioni 6.5.
Alisema uchaguzi wa Mikoa ya Songwe na Kigoma umezingatia Hali ya Upatikanaji wa Nishati ya Umeme uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu, 2020 na kuonesha kuwa mikoa ya Kigoma na Songwe ndiyo mikoa iliyokuwa na kiwango cha chini zaidi cha upatikanaji wa umeme.
Mradi unatarajiwa kuanza rasmi mwishoni mwa mwezi Machi 2023 baada ya kukamilika taratibu za manunuzi ya kupata wakandarasi watakaotekeleza mradi huo.
Mradi mwingine ni wa kupeleka umeme pembezoni mwa miji (Peri Urban) Awamu ya Pili ambapo alieleza kuwa ujenzi wa miundombinu ya Mradi huo kwa Mkoa wa Arusha, Dodoma na Mwanza umekamilika kwa asilimia 89.80 na kwamba maeneo 11 kati ya 150 yameunganishwa na umeme, wateja 9,252 kati ya 16,328 sawa na asilimia 57 wameunganishiwa umeme.
Alitaja gharama ya mradi kuwa ni shilingi bilioni 31.33 ambapo unaendelea kutekelezwa na unatarajiwa kukamilika mwezi Aprili 2023.
Mradi wa kupeleka umeme pembezoni mwa miji Awamu ya Tatu ni mwingine uliotolewa taarifa ambapo ilielezwa kwamba unatekelezwa kwa Mikoa 8 ya Geita, Kigoma, Kagera, Mbeya, Mtwara, Singida, Tabora na Tanga ambapo hadi kufikia Disemba 2022, wakandarasi wanne wamesaini mikataba ya kutekeleza mradi katika mikoa 6 na kwa sasa wapo maeneo ya mradi kuendelea na kazi za usanifu na manunuzi ya vifaa.
Aidha, ilielezwa kuwa Wakala upo katika hatua za mwisho kukamilisha mikataba kwa mikoa ya Geita na Kigoma na kwamba gharama ya Mradi ni shilingi bilioni 76.9 zitakazolipwa na Serikali ya Tanzania kwa asilimia 100. Jumla ya maeneo 416 na wateja wa awali 22,105 watanufaika na huduma ya umeme kutokana na Mradi huo unaotarajiwa kutekelezwa kwa miezi 18.
Aidha, Mradi mwingine ni unaohusu kupeleka umeme katika maeneo 336 ya uchimbaji mdogo wa madini, maeneo ya uwekezaji wa viwanda na mashamba ya Kilimo Tanzania Bara.
Ilielezwa kuwa Mradi huu unatarajiwa kuunganisha wateja wa awali 17,385 ambapo hadi kufikia Disemba 2022, Ununuzi wa Wakandarasi ulikuwa umekamilika na taratibu za kusaini mikataba zinaendelea. Mradi utatekelezwa kwa kipindi cha Miezi 9.
Kuhusu Mradi wa kusambaza umeme katika vituo vya afya na pampu za maji, Mhandisi Olotu alieleza kuwa unahusu kusambaza umeme katika Vituo vya Afya 59 na Pampu za Maji 333 vilivyoko vijijini.
Alisema Wakala umesaini mikataba na wakandarasi wanne kwa ajili ya kutekeleza kazi hizo katika Mafungu 7 ya Mradi kwa gharama ya shilingi bilioni 27.2.
Aidha, alifafanua kuwa, Mikataba ya utekelezaji wa miradi hiyo ilisainiwa tarehe 21 Novemba 2022 ambapo hadi kufikia Disemba 2022, Wakandarasi wameendelea na kazi ya upimaji wa njia za umeme, usanifu wa kina na kuandaa michoro ya usanifu mradi. Alisema Mradi unatarajiwa kukamilika Agosti 2023.
Pia, alizungumzia miradi ya kusambaza umeme vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili kwenye mikoa 24 ya Tanzania Bara ambayo inahusisha kupeleka umeme kwenye vijiji 4,071 kulingana na matokeo ya usanifu wa kina pamoja na kujenga miundombinu ya Msongo wa Kati yenye urefu wa kilomita 23,522, kujenga miundombinu ya msongo mdogo yenye urefu wa kilomita 4,082 kufunga mashine umba 4,071 na kuunga wateja wa awali wapatao 89,282.
Alieeleza kuwa gharama za mradi huo ni shilingi trilioni 1.24 ambapo hadi kufikia Disemba 2022, mafungu 10 wastani wa utekelezaji wa mradi umefikia zaidi ya asilimia 60. Mafungu matano utekelezaji upo kati ya asilimia 50 hadi asilimia 60 na mafungu 13 utekelezaji ni kati ya asilimia 40 hadi asilimia 50 na mafungu 11 yaliyobaki utekelezaji wake upo kati ya asilimia 20 hadi asilimia 40.
Mhandisi Olotu alihitimisha kwa kuelezea tathmini ya utekelezaji wa mradi ambayo inaonesha mkandarasi M/s STEG International Limited amekamilisha ujenzi wa miundombinu yote ya mradi kwa asilimia 100 kabla ya muda wa mradi kukamilika kwa fungu 30 katika wilaya za Meatu na Maswa katika mkoa wa Simiyu na fungu 18 katika Wilaya ya Morogoro vijijini katika Mkoa wa Morogoro.
Alisema ili kuhakikisha wananchi wengi wanaunganishwa na huduma ya umeme, Wakala umeongeza wigo wa njia za msongo mdogo kwa kilomita 2 pamoja na wateja 42 kwa kila kijiji.