Mkurugenzi wa Kampuni ya Songoro Marine Transport Limited Major Songoro akitoa taarifa ya ujenzi wa Vivuko vitatu vinavyojengwa kwenye Kalakana yake katika hafla ya uzinduzi wa Vivuko hivyo
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Adam Malima akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa ujenzi wa Vivuko vitatu vinavyojengwa na Kampuni kongwe ya kizalendo Songoro Marine Transport Limited
Mkurugenzi wa Kampuni ya Songoro Marine Major Songoro (wakwanza kulia) akiwapa viongozi maelezo mbalimbali ya namna wanavyoendelea kutekeleza ujenzi wa vivuko
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Adam Malima (kushoto) akichomelea vyuma ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa Vivuko vitatu vinavyojengwa na Kampuni ya Songoro Marine (kulia) ni Major Songoro
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Adam Malima (wakwanza kushoto) akipewa maelekezo na Mkurugenzi wa Kampuni ya Songoro Marine (kulia) namna ya kuchomelea vyuma ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa ujenzi wa Vivuko
Wafanyakazi wa Kampuni ya Songoro Marine wakiwa kwenye hafla ya uzinduzi wa ujenzi wa Vivuko vitatu
Muonekano wa awali wa Kivuko kimoja kati ya vitatu vinavyojengwa kwenye Kalakana ya Songoro Marine Transport Limited Jijini Mwanza
********************
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Adam Malima amezindua ujenzi wa Vivuko vitatu vitakavyotoa huduma katika maeneo ya Nyakarilo – Kome,Bwiru – Bukondo na Ijinga – Kahangala.
Hafla ya uzinduzi huo imefanyika leo Alhamisi Januari 26,2023 kwenye Kalakana ya Songoro Marine ambapo ujenzi huo unaendelea kutekelezwa.
Akizungumza kabla ya uzinduzi Mh.Malima amewataka wahusika kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wakati na kwa viwango vya juu ili kutimiza adhima ya Serikali kuwaondolea adha ya usafiri Wananchi.
” Kipekee naishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwauwekezaji mkubwa unaoenda kuondoa kero ya usafiri kwa wananchi wa Mkoa wa Mwanza na watanzania kwa ujumla, niimani yangu kuwa uwekezaji huu utainua hali za kiuchumi”, amesema Malima.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa Vivuko hivyo Mkurugenzi wa Kampuni ya Songoro Marine, Major Songoro amesema Kivuko cha Bwiro – Bukondo kitakuwa na upana wa mita 10 kitakuwa na uwezo wa kubeba Tani 100 ambazo ni sawa na abiria 200 na magari madogo 10.
Kwa upande wa Kivuko cha Ijinga – Kahangala Songoro ameeleza kuwa kitakuwa na upana wa mita 10 kitabeba abiria 200 pamoja na magari madogo 10.
Akizungumzia Kivuko cha Nyakarilo – Kome amesema kinaupana wa mita 12.5 kitakuwa na uwezo wa kubeba Tani 170 sawa na abiria 800 pamoja na magari madogo 22.
” Tumejipanga kikamilifu kuhakikisha Vivuko vinakamilika kwa muda uliopangwa ambao ni Julai 2023,pia natumia fursa hii kumshukuru Rais wa Jamuhri ya Muungano wa Tanzania kwakuendelea kuwaamini wakandarasi wazawa kwa kuwapatia miradi ya kimaendeleo”, amesema Songoro.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala wa ufundi na umeme Tanzania (TEMESA), Lazaro Kilahala amesema Vivuko hivyo vinajengwa kwa viwango vya Kimataifa (IMO Standards) ambavyo kwa hapa nchini vinasimamiwa na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kuanzia hatua ya usanifu hadi siku Kivuko kinaanza kutoa huduma.
Kilahala ameeleza kuwa kukamilika kwa ujenzi wa Vivuko hivyo kutawapatia wananchi wa maeneo hayo na watanzania kwa ujumla uhakika wa usafiri na hivyo kuchochea ukuaji wa shughuli zao za kiuchumi.
Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Ludovick Nduhiye, amewasihi Wananchi kuhakikisha wanavilinda Vivuko hivyo sanjari na kujiepusha na uharibifu wa mazingira yanayozunguka eneo la Vivuko ambao huathiri mifumo ya uendeshaji wa vyombo hivyo.
Awali akizungumza kwenye hafla hiyo Mbunge wa Jimbo la Buchosa Erick Shigongo, amesema Kome ni kisiwa ambacho kina wavuvi,wakulima wengi hivyo kuwepo kwa Kivuko kikubwa kitasaidia kuondoa kero ya usafiri kwa wananchi na uchumi wao utakuwa kwa kasi.