Mkurugenzi Mtendaji HakiElimu Dkt. John Kalagea (katikati) akizungumza na Waandishi wa habari akitoa tamko kuhusiana na adhabu ya viboko shuleni leo Januari 26,2023 Jijini Dar es Salaam
Mkurugenzi Mtendaji HakiElimu Dkt. John Kalage (katikati) akisisitiza jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 26,2023 Jijini Dar es Salaam
Mkurugenzi Mtendaji HakiElimu Dkt. John Kalage akisisitiza jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 26,2023 Jijini Dar es Salaam
Mshauri wa Masuala ya Elimu- HakiElimu, Dkt.Wilberforce Meena ( wa pili kulia) akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 26,2023 Jijini Dar es Salaam.
Mshauri wa Masuala ya Elimu- HakiElimu, Dkt.Wilberforce Meena akisisitiza jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 26,2023 Jijini Dar es Salaam.
(PICHA ZOTE NA EMMANUEL MBATILO)
*******************
NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
Shirika lisilo la kiserikali linaloshughulikia masuala ya elimu nchini, Haki Elimu limetoa wito kwa Serikali kuchukua hatua ambazo zitakomesha matumizi ya adhabu za viboko shuleni na kuhimiza adhabu chanya/adhabu mbadala ambazo sio za kikatili.
Wito huo umetolewa leo Januari 26,2023 Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji HakiElimu Dkt. John Kalage wakati akizungumza na Waandishi wa habari akitoa tamko kuhusiana na adhabu ya viboko shuleni.
Dkt.Kalage amesema rai yao vipengele vya Sheria ya Elimu ya Mwaka 1978, Mwongozo wa Elimu Juu ya Adhabu za Viboko wa Mwaka 2002 na Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009; vipitiwe upya ili kukataza kabisa matumizi ya viboko shuleni na kuzuia adhabu nyingine ambazo zinaweza kutoa mwanya wa ukatili kwa watoto kufanyika.
“Pamoja na kuwa madhara ya adhabu yameelezwa vizuri kwenye mafunzo ya taaluma ya ualimu ikiwemo maumivu ya aina mbalimbali kwa mtoto, kujenga chuki na hata kupunguza motisha ya kujifunza au kwenda shule, bado sehemu kubwa ya walimu wanaona matumizi ya viboko ndio njia rahisi na yenye ufanisi kuhakikisha nidhamu shuleni na kuhimiza watoto kujifunza kwa bidii”. Amesema Dkt.Kalage.
Amesema Walimu wanasisitiziwa kutumia mbinu mbadala katika kusimamia nidhamu ya wanafunzi. Kwa mfano wanashauri kutumia vichocheo hasi ili kuwafanya wanafunzi wasiendelee na mwenendo ambao haufai badala ya adhabu ikiwemo adhabu ya viboko.
“Hata hivyo, matumizi ya njia mbadala kusimamia nidhamu yanategemea sana uwezo wa walimu katika kuzitumia. Kinachojitokeza wazi ni kwamba walimu wengi wanashidwa kutumia njia mbadala na kwa sababu sharia na miongozo inaruhusu viboko basi wanachagua viboko badalla ya vichocheo hasi”. Amesema
Pamoja na hayo wamepokea kwa masikitiko taarifa ya tukio la adhabu ya kikatili waliyoipata mwanafunzi wawili wa Shule ya msingi Kakanja iliyopo Wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera. Tukio hilo lilitekelezwa na Mwalimu Mkuu wa shue hiyo Isaya Benjamini ambaye anaonekana kwenye kipande kifupi cha video akiwacharaza bakora kwenye nyayo za miguu wanafunzi wawili
“Tunaamini kitendo hiki kinakiuka sio tu haki za Watoto bali pia ni kinyume na maadili ya kazi ya ualimu na malezi bora ya wanafunzi”. Ameeleza.
Hata hivyo wameipongeza Serikali kupitia Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia na uongozi wa Mkoa wa Kagera kwa kuchukua hatua za haraka na za awali dhidi ya mwalimu aliyehusika na ukatili huo ikiwa ni pamoja na kumvua nafasi yake ya Ualimu Mkuu, kumsimamisha kazi na kuunda tume ya kuchunguza tukio hilo ili hatua za kisheria ziweze kufuata.
Amesema katika utafiti uliofanywa na Shirika la HakiElimu Mwaka 2020; takribani 87.9% ya Watoto wa shule waliripoti kufanyiwa ukatili wa kimwili huku asilimia 90% kati ya hao walisema ukatili wa kimwili waliofanyiwa ulitokana na adhabu za viboko zinazotolewa shuleni. Katika utafiti huu, asilimia 54.9% ya Watoto walisema walimu wao na walezi wanatumia kupiga ngumi na makofi kama sehemu ya adhabu.