Mratibu wa kifua kikuu na ukoma wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Dkt Mkasange Kihongole akielezea kampeni za kupambana na kifua kikuu zinavyoendelea.
Mganga Mkuu wa wilaya ya Tunduru Dkt Wilfred Rwechungura kushoto,akipitia taarifa za hali ya ugonjwa wa kifua kikuu katika wilaya hiyo,kulia mratibu wa kifua kikuu na ukoma Dkt Mkasange Kihongole.
Mratibu wa kifua kikuu na ukoma wa wilaya ya Tunduru Dkt Mkasange Kihongole katikati akiwa na mkazi wa kijiji cha Mchuruka wilayani humo Salum Jawabu kulia ambaye amemaliza kutumia dawa za ugonjwa wa kifua kikuu,kushoto ni mke wa Jawabu Bi Mwanahawa Wadali.
……………………………..
Na Muhidin Amri,Tunduru
HOSPITALI ya wilaya Tunduru mkoani Ruvuma,kupitia kitengo cha kifua kikuu na ukoma imefanikiwa kuibua jumla ya wagonjwa 1,028 sawa na asilimia 122.2 kati ya lengo la kuibua wagonjwa 841 hadi kufikia mwezi Disemba mwaka 2022.
Hayo yamesemwa na Mganga Mkuu wa wilaya hiyo Dkt Wilfred Rwechugura,wakati akitoa taarifa ya kampeni dhidi ya mapambano ya ugonjwa wa kifua kikuu inayofanyika katika vijiji mbalimbali wilayani humo kwa mwaka 2023.
Dkt Rwechungura alisema,kati ya hao wagonjwa 70 sawa na asilimia 6.8 walikutwa na maambukizi ya VVU ambapo watoto walio chini ya umri wa miaka kumi na tano waliokutwa na vimelea vya ugonjwa wa kifua kikuu ni 245 sawa na asilimia 23.8.
Kwa mujibu wa Dkt Rwechungura,watoto chini ya miaka mitano wanaoishi na wagonjwa wa kifua kikuu waliochunguzwa na kupimwa 196 na walioanza dawa kinga185,wanaoishi na wagonjwa wa TB na wakabainika kupatwa na ugonjwa huo ni 17 na waliofariki dunia 17 sawa na asilimia 1.6.
“kimsingi ugonjwa wa kifua kikuu katika wilaya yetu bado ni tatizo kubwa,hata hivyo tunaendelea na mapambano kupitia kampeni zinazofanyika katika maeneo mbalimbali,lengo letu ni kutokemeza kabisa ugonjwa huo”alisema.
Alisema,tatizo la ugonjwa wa kifua kikuu katika wilaya hiyo linatokana na uwepo wa machimbo ya madini ambayo yana mkusanyiko wa watu wengi, hivyo ni rahisi kuambukizana pamoja na ukosefu wa nyumba bora hasa maeneo ya vijijin.
Dkt Rwechungura, ameitaka jamii kujenga nyumba bora zenye uwezo wa kuingiza hewa ya kutosha na wale watakaona dalili za ugonjwa huo ni vyema kuwahi katika vituo vya kutolea huduma kwa ajili ya uchunguzi badala ya kukaa nyumbani au kukimbilia kwa waganga wa tiba asili.
Alieleza kuwa,katika kipindi hicho watu waliogundulika na ugonjwa wa ukoma ni 85 waliopima VVU ni 85 sawa na asilimia 100 na hakuna aliyebainika kupata virusi vya ukimwi.
Aidha alisema, katika kipindi hicho watu wanaoishi na wagonjwa wa Ukoma na wakachunguzwa walikuwa 52,ambapo hakuna aliyegundulika kuwa na ugonjwa huo na wagonjwa wa ukoma waliopata viatu ni 29 na wagonjwa 37 wana ulemavu wa kudumu.
Amewashukuru wadau wanaotoa huduma za afua mbalimbali za afya zikiwamo za kifua kikuu,ukimwi na ukoma ambao wamekuwa washiriki wazuri katika kuhakikisha afya za wananchi wa wilaya hiyo zinaimarika.
Kwa upande wake Mratibu wa kifua kikuu na ukoma wa wilaya hiyo Dkt Mkasange Kihongole alisema,kwa mwaka 2023 serikali kupitia wizara ya afya imewapa malengo ya kuibua wagonjwa 874.
Alisema,Halmashauri ya wilaya Tunduru kwa kushirikiana na Wizara ya Afya kupitia mkakati wa kudhibiti kifua kikuu na ukoma itahakikisha dawa za kutibu kifua kikuu zinapatikana wakati wote na zinatolewa bila malipo na kuimarisha uwezo wa vituo vya ugunduzi wa TB.
Alitaja mikakati itakayofanikisha kuwapata wagonjwa hao ni kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu ugonjwa huo unavyoenea,dalili na namna ya kujikinga na maeneo yatakayohusika ni shule za msingi na sekondari za kutwa na bweni.
Mkasange alitaja mkakati mwingine ni kuhakikisha familia zote zinazoishi na wagonjwa wa TB zinafanyiwa uchunguzi na wale watakaobainika wataanzishiwa matibabu yanayotolewa bila malipo(bure)kwenye vituo vyote vya kutolea huduma za matibabu.
Alisema, katika kampeni hizo watashirikiana na wahudumu wa afya ngazi ya jamii wanaofanya kazi ya kusanya sampuli za makohozi na kuzipeleka Hospitali kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi kwa kutumia mashine za kupimia sampuli za makohozi yaani Gene-Xpert.
Amewataja wadau wengine watakaoshirikiana nao kwenye mapambano ya kifua kikuu ni pamoja na shirika lisilo la Kiserikali la MDH na vyombo vya Habari ambavyo vina mchango na nafasi kubwa ya kupeleka elimu ya ugonjwa huo kwa jamii.
Dkt Mkasange,amewaonya waganga wa tiba asili na tiba mbadala,kuacha tabia ya kuwakumbatia wateja wenye dalili za kifua kikuu ili kuepuka uwezekano wa kuambukizwa wao wenyewe na wateja wanaofika kwenye vilinge vyao.
Mkazi wa mtaa wa Nakayaya Yusufu Juma anayeugua ugonjwa wa kifua kikuu,amewashukuru wataalam wa kitengo cha kifua kikuu katika Hospitali ya wilaya kwa huduma nzuri ambazo zimesaidia kuokoa maisha yake na watu wengine.
Salum Jawabu mkazi wa Mchuruka aliyemaliza dawa za kifua kikuu na kupoma,amewaomba watu waliobainika kuwa na TB na kuanzishiwa matibabu kuendelea kumeza dawa badala ya kukimbia kwani kufanya hivyo ni hatari kwa maisha yao.
Alisema,ugonjwa huo unatibika kwa mgonjwa kumeza dawa kila siku na kuepuka kukimbilia kwa waganga wa tiba asili na tiba ambao hawana vipimo na tiba sahihi za ugonjwa wa kifua kikuu.