Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Utawala na Rasilimali Watu (sehemu ya rasilimali watu), Bw. Benjamin Chilumba, akifungua Kongamano la Siku mbili la Wakuu wa Vitengo vya Mawasiliano wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Jenifa Omolo, linalofanyika mkoani Morogoro.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Benny Mwaipaja akisema jambo wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Siku mbili la Wakuu wa Vitengo vya Mawasiliano wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango linalofanyika mkoani Morogoro.
Baadhi ya Wakuu wa Vitengo vya Mawasiliano wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango wakisiliza kwa umakini mada mbalimbali wakati Kongamano la Siku mbili la Wakuu wa Vitengo vya Mawasiliano wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango linalofanyika mkoani Morogoro.
Baadhi ya Wakuu wa Vitengo vya Mawasiliano wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango wakisiliza kwa umakini mada mbalimbali wakati Kongamano la Siku mbili la Wakuu wa Vitengo vya Mawasiliano wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango linalofanyika mkoani Morogoro.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Bw. Innocent Primus Mungy akitoa mada kwa jambo wakati wa kongamano la Siku mbili la Wakuu wa Vitengo vya Mawasiliano wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango linalofanyika mkoani Morogoro.
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Utawala na Rasilimali Watu, Bw. Benjamin S. Chilumba (katikati waliokaa), Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Benny Mwaipaja (wapili kushoto waliokaa), Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Bw. Innocent Primus Mungy (wapili kulia waliokaa) wakiwa katika picha ya pamoja na Wakuu wa Vitengo vya Mawasiliano wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango wakati wa Kongamano la Siku mbili linalofanyika mkoani Morogoro.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango-Morogoro)
……………………………………..
Na. Saidina Msangi, WFM, Morogoro
Wakuu wa Vitengo vya Mawasiliano wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango wametakiwa kuwasiliana kimkakati ili kufikisha taarifa zinazohusiana na Wizara pamoja na Taasisi zake kwa wananchi kwa kuzingatia viwango na kwa wakati.
Rai hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Jenifa Omolo, ambaye aliwakilishwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Utawala na Rasilimali Watu (sehemu ya rasilimali watu), Bw. Benjamini Chilumba, katika ufunguzi wa kongamano la Wakuu wa Vitengo vya Mawasiliano wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango, lililofanyika mkoani Morogoro.
Alisema kuwa kongamano hilo litatoa fursa kwa washiriki kujadili changamoto zinazowakabili ili kuzipatia ufumbuzi utakaoongeza utendaji kazi na ufanisi katika majukumu ya kila siku kwa maendeleo ya Wizara na Taifa kwa ujumla.
Alisema kuwa ushiriki katika kongamano hilo ni ishara njema kwa ustawi wa Wizara na Taasisi zake katika kukuza na kuimarisha Mawasiliano kwa Umma na kuwa michango, ushauri na mapendekezo yatakayotolewa kupitia majadiliano yatafanyiwa kazi ili kuboresha zaidi Kongamano lijalo pamoja na kuendeleza mahusiano mazuri ya kimawasiliano kati ya Wizara na Taasisi zake.
‘‘Ninawaagiza Wakuu wa vitengo vya mawasiliano wote kuendelea kutumia jukwaa hili kujadili na kubadilishana uzoefu wa masuala mbalimbali ya Mawasiliano ya Umma na usambazaji wa taarifa kwa wadau wetu, ni matumaini yangu kuwa siku za usoni kongamano hili litakuwa ni miongoni mwa makongamano bora na makubwa zaidi nchini’’, alisema Bw. Chilumba.
Alitoa rai kuwa kongamano hilo ambalo ni la kwanza kufanyika katika siku zijazo lishirikishe wadau wengi zaidi wa mawasiliano ili kuweza kupata mawazo tofauti na kujenga mahusiano mazuri na wadau hao kwa lengo la kuitangaza Wizara, Taasisi zake na Serikali kwa jumla.
Awali Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Benny Mwaipaja, alisema kuwa kutokana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia sekta ya mawasiliano imebadilika hivyo kongamano hilo litatoa fursa kwa washiriki kujadili, kujenga ukaribu na kukumbushana mambo muhimu ya mawasiliano na wadau ndani na nje ya taasisi za wizara.
‘‘Mawasiliano ya kimkakati yatatuwezesha sisi kama Wizara na Taasisi zake kutoa taarifa sahihi, kwa wakati na zilizochambuliwa vizuri’’, alisisitiza Bw. Mwaipaja.
Alisema kwa kuzingatia mabadiliko katika sekta ya mawasiliano kongamano hilo litasaidia kubadilishana mawazo na kujipanga kimkakati namna ya kutoa taarifa za Wizara na taasisi zake kwa umma.
Mada mbalimbali zilitolewa na wataalamu wa masuala ya Mawasiliano ili kuwajengea uwezo Wakuu wa Vitengo vya Mawasiliano katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku ikiwemo jinsi ya kufanya mawasiliano ya umma kimkakati na njia bora ya matumizi ya mtandao ya jamii katika kufikisha taarifa za Serikali na Taasisi zake umma.
Kongamano hilo lilihudhuriwa na wakuu wa vitengo vya mawasiliano vya taasisi zilizo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango ikiwemo, Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA), Mfuko wa Self Microfinance, Bodi ya Wataalamu wa Ugavi na Ununuzi Tanzania (PSPTB), Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP), Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA, Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR), Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika (EASTC), Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Taasisi ya Uhasibu Arusha (AII), Mfuko wa Uwekezaji wa UTT, Hazina Saccoss, Mamlaka ya Rufaa ya Zabuni za Umma (PPAA) na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA).