Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akizungumza kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan na Wanawake wamiliki wa shule na vyuo vya kati nchini (TAWOSCO) wakati wa uzinduzi wa umoja huo Januari 20, 2023 Jijini Dar es salaam.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akisalimiana na baadhi ya viongozi wa umoja wa Wanawake wamiliki wa shule na vyuo vya kati nchini (TAWOSCO) kabla ya kuzindua umoja huo Kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan Januari 20, 2023 Jijini Dar es salaam
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wamiliki wa shule na vyuo vya kati nchini (TAWOSCO) Bi. Justina Lukumay akieleza jambo wakati wa hafla ya uzinduzi wa Umoja wa Wanawake hao, Januari 20, 2023 Jijini Dar es salaam.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Umoja wa Wanawake wamiliki wa shule na vyuo vya kati nchini (TAWOSCO), Januari 20, 2023 Jijini Dar es salaam.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akipokea zawadi ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alipomwakilisha kuzindua umoja wa Wanawake wamiliki wa shule na vyuo vya kati nchini (TAWOSCO) January 20, 2023 Jijini Dar es salaam.
Wanawake wamiliki wa shule na vyuo vya kati nchini wakifuatilia matukio katika uzinduzi wa umoja huo uliofanywa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima kwa niaba ya Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Januari 20, 2023.
…………………………..
Na WMJJWM, DSM
Wanawake wamiliki wa shule na vyuo vya kati wametakiwa kuwa mstari wa mbele kupambana na ukatili kwa watoto hasa shuleni kwa kuanzisha na kuendesha madawati ya ulinzi kwa ufanisi kwa kuzingatia miongozo ya madawati hayo.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ametoa rai hiyo kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, wakati akizindua Umoja wa Wanawake Wamiliki wa shule na vyuo vya kati nchini (TAWOSCO) Januari 20, 2023 jijini Dar es Salaam.
Dkt. Gwajima amewataka wamiliki hao kuhakikisha shule na vyuo vinakuwa na madawati ya ulinzi shuleni na ya Jinsia vyuoni ili kuwalinda watoto dhidi ya ukatili.
“Wizara ninayoisimamia ina dhamana ya kuandaa miongozo kuhusu maendeleo yanayohusu Wanawake na Watoto. Mojawapo ya eneo la miongozo ni kuhusu ulinzi na usalama kwa Watoto ambapo, Wizara imeandaa Mwongozo wa Uanzishwaji na Uendeshaji wa Dawati la Ulinzi na Usalama wa Mtoto ndani na nje ya Shule” Amesema Waziri.
Amesema Mwongozo huo unalenga kuhakikisha watoto wanapata ulinzi dhidi ya vitendo vya ukatili na hadi sasa jumla ya madawati 585 yameanzishwa Tanzania nzima.
“Hivyo, mkiwa ni Wamiliki wa Shule na Vyuo zaidi ya 1000 na zenye wanafunzi takribani milioni moja (1,000,000), nyie ni wadau wakubwa kwenye utekelezaji wa ulinzi wa watoto shuleni, sasa niwaombe kupitia mwongozo huu mkaanzishe madawati haya ya ulinzi na usalama kwenye shule zenu ili kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya watoto mashuleni na ifikapo Februari, 2023 nipate taarifa” amesisitiza Waziri Gwajima.
Ametoa rai kwa vyuo vyote nchini kuanzisha madawati ya Jinsia kwenye vyuo vya elimu ya juu na kati kwani idadi ya madawati yaliyopo hadi sasa ni 37.
Aidha, Waziri Dkt. Gwajima amewaelekeza wamiliki hao kuzingatia waraka namba 24 wa viboko shuleni wa Mwaka 2020
kwa kutoruhusu adhabu zeye madhara kwa watoto kwani zikizidi vigezo ni sehemu ya ukatili.
Halikadhalika, Waziri Gwajima ameendelea kusisitiza suala la magari ya Watoto ya shule hasa binafsi kuhusika na matukio ya ukatili kwa watoto amewata wamiliki hao kutosubiri matamko au sera kuzuia suala hilo na kuwataka kuhakikisha kuajiri watoa huduma wa kike katika magari hayo. Amehimizia wasisubiri matukio ndipo waone umuhimu.
Amewapongeza Wanawake wamiliki wa shule na vyuo kwa ubunifu wa kuungana kwa lengo la kuunga mkono juhudi za Serikali na kuongeza nguvu katika kuimarisha Elimu kwa kuhakikisha kila mtoto anapata Elimu na kuwahakikishia kuzifikisha changamoto zao kwa Rais Samia Ili zipatiwe ufumbuzi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa TAWOSCO Bi. Justina Lukumay akisoma risala ya Umoja huo amesema lengo la Umoja huo ni kuchangia jitihada za Serikali pamoja na wadau mbalimbali katika kuhakikisha kila Mtoto mwenye umri wa kwenda shule anapatiwa nafasi hiyo.
Ameiomba Serikali kuzitatua changamoto za Umoja huo ili waweze kufikia Jamii kubwa zaidi katika kutekeleza malengo yake.
Naye Afisa Elimu Mkoa wa Dar es salaam Bw. Abdul Maulid amemhakikishia Waziri Gwajima kuwa mkoa unatekeleza maelekezo ya kila shule yenye usafiri kuajiri watumishi wa kike, dhamira ikiwa ni kulinda watoto wa Kitanzania.