Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye leo Januari 20, 2023 amekagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la Wiraza anayoisimamia lililopo katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.
…………………………
Idara ya Habari – MAELEZO
Ujenzi wa jengo la Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari unatarajiwa kukamilika Oktoba 2023 hivyo kuongeza ufanisi wa wizara hiyo katika kuwahudumia Watanzania.
Akizungumza leo jijini Dodoma baada ya kukagua ujenzi wa jengo hilo linalojengwa katika Mji wa Serikali – Mtumba, waziri wa wizara hiyo, Mhe. Nape Nnauye amesema atatoa ushirikiano pale ujenzi utakapokwama.
“Nimekuja kutembelea baada ya kuona kasi ya ujenzi inapungua, nataka kasi iongezeke,” ameelekeza Mhe. Nape.
Pamoja na hilo, Msimamizi wa Mradi kutoka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Mhandisi Grace Musita amesema ujenzi ulitakiwa kukamilika Aprili 2023 lakini umechelewa kutokana na changamoto mbalimbali ikiwamo ugumu wa ardhi, kupanda kwa gharama za ujenzi na kuchelewa kupata michoro ya miundombinu ya mfumo wa majitaka.
“Mradi ulianza kutekelezwa mwaka 2021 kwa gharama ya shilingi bilioni 23.9, tumeshalipwa shilingi bilioni 7.9 tu, ujenzi umefikia asilimia 59.5 na tumefwata taratibu zote za ujenzi kwa kupima vifaa vyote vya ujenzi,” ameeleza Mhandisi Musita.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa Jengo, Ndg. S.H Mvunye amesema jengo hilo litakuwa na muonekano wa ghrofa tano na moja ya chini (basement).