Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Khamis Hamza Chilo,akizungumza leo na baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Mikwese,wilayani Manyoni,mkoani Singida ambako mradi wa bwawa wa Kupambana na atahari za Mabadiliko ya Tabia nchi unaendelea huku akiwataka wananchi hao kutunza miradi hiyo.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Khamis Hamza Chilo, akipanda mti katika eneo la mradi wa bwawa wa Kupambana na athari za Mabadiliko ya Tabia nchi, uliopo katika Kijiji cha Mikwese, wilayani Manyoni, mkoani Singida.
Mkuu wa Wilaya ya Manyoni,Rahabu Mwagisa akipanda mti katika eneo la mradi wa bwawa wa Kupambana na athari za Mabadiliko ya Tabia nchi, uliopo katika Kijiji cha Mikwese, wilayani Manyoni, mkoani Singida.Picha na OMR
………………………………
Na Mwandishi Maalumu
Serikali imetoa agizo la ushirikishwaji wananchi katika miradi ya kupambana na mabadiliko ya tabia nchi huku ikisisitiza uelewa mzuri wa miradi hiyo itasaidia wananchi kuwa mabalozi wa kupambana na athari na uharibifu wa mazingira katika maeneo mbalimbali nchini.
Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Khamis Hamza Chilo alipotembelea mradi wa kupambana na mabadiliko ya tabia nchi uliopo katika Kijiji cha Mikwese,wilayani Manyoni mkoani Singida ambapo unajumuisha uchimbwaji wa bwawa kubwa litakalotumika kumwagilia miti itakayopandwa katika maeneo yaliyoathirika na mabadiliko ya tabia nchi huku pia maji hayo yakitumika kuendesha kilimo cha mbogamboga na shughuli za ufugaji.
“Serikali inatoa fedha nyingi katika miradi hii ya kupambana na mabadiliko ya tabia nchi na madhara ya mabadiliko ya tabia nchi wanaoathirika ni wananchi,hivyo naagiza uwepo ushirikishwaji wa wananchi katika miradi hiyo,ushirikishwaji huo utasaidia wananchi hao kuwa mabalozi wa kutunza mazingira” alisema Naibu Waziri,Khamis Hamza Chilo
Akizungumza katika ziara hiyo,Mbunge wa Manyoni Mashariki,Dkt. Pius Chaya ameomba uwepo wa ubadilishanaji taarifa kuhusu mradi huku akisisitiza ushirikishwaji wa wananchi katika miradi hiyo.
“Binafsi mimi kama mbunge ambae ndiye mwakilishi wa wananchi sina taarifa sahihi za mradi huu sijashirikishwa,nawaomba watekelezaji wa mradi huu waje kwenye baraza la madiwani watuelezee kuhusu mradi huu,miradi hii imegharimu fedha nyingi lazima tushirikishwe viongozi ili tuweze kujua pia thamani ya fedha”alisema Dkt.Chaya
Akizunngumza pia katika ziara hiyo Mkuu wa Wilaya ya Manyoni,Rahabu Mwagisa amewataka wananchi kuikubali miradi hiyo pasina kuihujumu kwani inatumia fedha nyingi ambazo serikali imeona ni vema kuwaokoa wananchi wake na athari za uharibifu wa mazingira unaosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi.
Mradi huo una gharama ya shilingi Bilioni 3/- ukijumuisha na miradi mingine kama hiyo ya Kupambana na Mabadiliko ya Tabia nchi iliyopo katika wilaya ya Bahi na Nzega huku watekelezaji wa mradi huo wakitoka Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine na ukisimamiwa na Baraza la Taifa la Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira(NEMC).