Waziri wa Nishati, Mhe.January Makamba (kushoto) akiwa na Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Mhe.Isaac Njenga (kulia) mara baada ya kumaliza mazungumzo kati yao kuhusu ushirikiano wa Tanzania na Kenya katika Sekta ya Gesi na Umeme katika Ofisi za Wizara ya Nishati jijini Dodoma.
Waziri wa Nishati, Mhe.January Makamba (kushoto) na Balozi wa Kenya nchini Tanzania,Mhe.Isaac Njenga (kulia) wakizungumza kuhusu ushirikiano wa Tanzania na Kenya katika Sekta ya Gesi na Umeme katika Ofisi za Wizara ya Nishati jijini Dodoma.
Waziri wa Nishati, Mhe.January Makamba (kushoto) akimsikiliza Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Mhe.Isaac Njenga (kulia) mara baada ya kufika katika Ofisi za Wizara ya Nishati jijini Dodoma ili kuzungumza masuala yanayohusu ushirikiano wa Tanzania na Kenya katika Sekta ya Gesi na Umeme.
Waziri wa Nishati, Mhe.January Makamba (kushoto) akizungumza na Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Mhe.Isaac Njenga (kulia) kuhusu masuala yanayohusu ushirikiano wa Tanzania na Kenya katika Sekta ya Gesi na Umeme katika Ofisi za Wizara ya Nishati jijini Dodoma. Wengine Katika picha ni Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Eng.Innocent Luoga na Kaimu Kamishna Msaidizi wa Gesi, Eng.Joyce Kisamo.
…………………………………….
Na Teresia Mhagama
Waziri wa Nishati, Mhe.January Makamba pamoja na
Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Mhe.Isaac Njenga
wamekutana na kufanya mazungumzo kuhusu ushirikiano
wa Tanzania na Kenya katika Sekta ya Umeme na Gesi.
Mazungumzo hayo yamefanyika tarehe 18 Januari, 2023
jijini Dodoma ambapo viongozi hao walizungumzia
ushirikiano katika kuendeleza nishati ya Jotoardhi, Jua,
Upepo pamoja na mradi ya usafirishaji Gesi, usafirishaji
umeme na usambazaji umeme vijijini.
Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba amemueleza
Balozi Njenga kuwa, Tanzania ipo tayari kuendeleza
ushirikiano na Kenya katika Sekta ya Gesi na Umeme
kwani nchi hizo tayari zina ushirikiano kwenye sekta
mbalimbali ikiwemo miundombinu ya barabara na anga.
Kuhusu mradi wa usafirishaji Gesi kutoka Tanzania
kwenda Kenya, amesema kuwa mradi huo ni wa
kipaumbele kwa viongozi Wakuu wa nchi hizo mbili na
kwamba tayari timu za majadilino kutoka Kenya na
Tanzania zimeshaundwa na zinaendelea na kazi ya
kuandaa nyaraka mbalimbali zitakazowezesha mradi huo
kusonga mbele.
Aidha, kuhusu ushirikiano kwenye Jotoardhi amesema
kuwa, Tanzania imeshaanza kuchukua hatua mbalimbali
za kuendeleza vyanzo hivyo ikiwemo za upatikanaji wa
fedha kutoka vyanzo vya ndani na nje ya nchi na kwamba
mtambo wa uchorongaji visima vya jotoardhi kwa ajili ya
kuendeleza Jotoardhi unatarajiwa kuwasili nchini mwezi
wa Pili mwaka 2023.
Vilevile, amesema Tanzania ipo tayari kushirikiana na
Kenya katika kuendeleza vyanzo vya umeme jadidifu
vikiwemo Jua na Upepo.
Kuhusu ushirikiano katika miradi ya umeme vijijini,
amesema kuwa, ushirikiano huo ni muhimu kwani
Tanzania na Kenya zitaweza kubadilishana uzoefu, na
hivyo kuweza kufikisha huduma ya umeme vijijini kwa
ufanisi zaidi.
Kwa upande wake, Balozi wa Kenya nchini Tanzania,
amemueleza Waziri wa Nishati kuhusu nia ya nchi hiyo
kushirikiana na Tanzania katika uendelezaji wa nishati ya
Jotoardhi kwani Tanzania ina vyanzo vya kutosha kuweza
kuzalisha umeme kwa kutumia Jotoardhi.
Amesema kuwa, Kenya tayari imeshapiga hatua katika
uendelezaji wa Jotoardhi kwani kwa sasa wanazalisha
takribani megawati 986 za umeme kwa kutumia nishati
hiyo ambayo ni asilimia 46 ya umeme wote unaozalishwa
nchini Kenya.
Aidha, Mhe.Balozi Isaac Njenga amemueleza Waziri wa
Nishati kuhusu utayari wa Kenya katika kutekeleza
makubaliano ya ushirikiano yaliyoingiwa kati ya nchi hizo
mbili kwenye mradi wa usafirishaji gesi kutoka Tanzania
na miradi ya usafirishaji wa umeme kwa msongo wa kV
400 ambayo itawezesha nchi hizo mbili kuweza kuuziana
umeme.
Vilevile, amemueleza Waziri wa Nishati kuhusu Kenya na
Tanzania kushirikiana katika miradi ya usambazaji umeme
vijijini hali itakayowezesha kila nchi kujifunza mbinu za
mafanikio ya usambazaji umeme vijijini.
Kwa upande wa Serikali ya Tanzania, kikao hicho
kilihudhuriwa na Kamishna wa Umeme na Nishati
Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga na Kaimu Kamishna
Msaidizi wa Gesi, Mhandisi Joyce Kisamo