Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako (katikati) akizindua kitabu maalum cha watu wasioona chenye maudhui ya usalama na afya mahala pa kazi mara baada ya kufungua rasmi mafunzo ya usalama na afya yaliyotolewa kwa wajasiriamali wasioona jijini Dodoma. Kulia ni Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Katiba na Sheria, Mhe. Yahya Masare (Mb), Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA), Bi. Khadija Mwenda. Kushoto ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Watu wenye Ulemavu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Bw. Rasheed Maftah na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wasioona, Bw. Omari Amas.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako (katikati) akimkabidhi Fimbo nyeupe na kitabu maalum cha watu wasioona chenye maudhui ya usalama na afya mahala pa kazi kwa mjasiriamali asiyeoona Bi. Fadhila William wakati wa mafunzo hayo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako akihutubia wajasiriamali wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya usalama na afya kwa watu wasioona yaliyofanyika katika jengo la OSHA, jijini Dodoma.
Sehemu ya watu wasioona wakisikiliza maelezo ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako (hayupo pichani) wakati wa hafla hiyo.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA), Bi. Khadija Mwenda akieleza jambo wakati wa mafunzo hayo.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wasioona, Bw. Omari Amas,akitoa taarifa wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya usalama na afya kwa watu wasioona yaliyofanyika katika jengo la OSHA, jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako akisalimiana na baadhi ya washiriki mara baada ya kuzindua mafunzo ya usalama na afya kwa watu wasioona yaliyofanyika katika jengo la OSHA, jijini Dodoma.
…………………………….
Na;.OWM – KVAU -DODOMA
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako ameutaka Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA) kuweka mkazo wa kukuza uelewa wa masuala usalama na afya kwa Watu wenye Ulemavu.
Prof. Ndalichako ameyasema hayo leo jijini Dodoma alipokuwa akifungua mafunzo ya usalama na afya kwa watu wasioona Mkoa wa Dodoma.
Amesema mafunzo OSHA imekuwa ikitekeleza program ya mafunzo kwa makundi mbalimbali ikiwamo wajasiriamali na wachimbaji wa madini na kwa mwaka 2022 walifikiwa watu 11,204.
“Niipongeze Taasisi ya OSHA kwa kuendelea kuona umuhimu wa kutoa mafunzo haya na kuandaa chapisho kwa ajili ya watu wasioona, naagiza hakikisheni mnachapisha nakala za kutosha na kuzisambaza mikoa mingine na haya mafunzo muendelee kutoa hata kwenye maeneo mengine ili kuwezesha wafanyakazi na Watu wenye Ulemavu kuzingatia masuala ya usalama na afya mahali pa kazi,” amesema.
Aidha, Waziri Ndalichako amesema masuala ya usalama na afya yana umuhimu sana katika maendeleo na ustawi wa watu duniani hivyo yanapaswa kupewa uzito unaostahili.
“Mathalani takwimu za Shirika la Kazi Duniani (ILO) za mwaka 2022, zinaonesha kuwa watu milioni 2.9 hupoteza maisha na wengine zaidi ya milioni 400 huumia kutokana na ajali na magonjwa yatokanayo na kazi duniani kote na Tanzania ikiwemo,” amesema.
Vile vile, Prof. Ndalichako amesema magonjwa na ajali zitokanazo na kazi huisababishia dunia hasara ya zaidi ya asilimia tano ya pato lake ghafi la mwaka na hivyo kuhimiza uwajibikaji ili kubadilisha hali hiyo kupitia mafunzo hayo ambayo ni nyenzo muhimu ya kutusaidia kupunguza ajali na magonjwa katika sehemu za kazi ili kuongeza tija kwenye uzalishaji.
Naye, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, amesema mafunzo hayo kwa watu wasioona ni utekelezaji wa mwongozo wa ujumuishwaji na uimarishwaji wa huduma kwa watu wenye ulemavu nchini na taasisi hiyo ina jukumu la kuimarisha usalama na afya kwenye shughuli zao.
“Pamoja na kutoa mafunzo leo tumekuja na fimbo 100 kwa ajili yao na tutawapatia na kitabu maalum kilichochapishwa kwa nukta nundu na tumetengeneza baada ya kutembelea maeneo yao ya kazi na kuona shughuli wanazofanya,”amesema.
Mwenda amesema watu wenye ulemavu wanapofanya kazi kwenye mazingira hatarishi kuna hatari ya kuongeza ulemavu na mafunzo hayo ni muhimu katika kutengeneza kinga ili hali hiyo isiongezeke.
“Tunawafundisha wenzetu hawa ili washiriki vyema kwenye shughuli za kiuchumi, kwa kuwa takwimu za ILO za mwaka 2017 inaonesha asilimia moja hadi saba ya pato la taifa la nchi yeyote hupotea kwa kukosekana ujumuisho wa watu wenye ulemavu, hivyo tukitengeneza miundombinu mizuri wana uwezo wa kuzalisha na pato likaonekana katika kujenga nchi,”amesema.
Awali, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wasioona, Bw. Omari Amas, amepongeza serikali kupitia OSHA kwa kuona umuhimu wa kuwapatia elimu hiyo ambayo itasaidia wajikwamue kiuchumi.
Kwa upande wake Mbunge wa Viti maalum, Mhe. Khadija Taya, amesema mafunzo hayo yataleta chachu kwa watu wenye mahitaji maalum kujikwamua kiuchumi na kuchangamkia fursa mbalimbali.