Na Mwamvua Mwinyi, Kisarawe
MAMENEJA wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) ,wameagizwa kusimamia fedha za miradi ya barabara zinazotolewa na Serikali na kuhakikisha wanaitekeleza kulingana na usanifu uliofanyika pasipo kuzitumia kwa matumizi mengine ,kinyume na hivyo ni kuihujumu Serikali.
Aidha wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo wanapaswa kufanya kazi kwa ufanisi ,kwa kiwango kinachotakiwa, kumaliza kazi kwa wakati kwa kuzingatia mikataba Yao .
Maagizo hayo yaliyolewa na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi-Ujenzi ,Mhandisi Godfrey Kasekenya akiwa Wilayani Kisarawe ,mkoani Pwani ,wakati alipokwenda kukagua ujenzi wa barabara ya Pugu – Manerumango yenye urefu wa km 60 itakayogharimu biln 7.88, ambayo ni kiunganishi cha Mbuga ya Selou na Bwawa la Mwalimu Nyerere na barabara ya kutokea Pugu hadi Mloka yenye urefu wa Km 157 .
Alieleza, Rais Samia Suluhu Hassan ametenga fedha nyingi kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya barabara, “Wizara haitegemei kuona barabara zikijengwa chini ya kiwango, na endapo mtafanya hivyo ni kuihujumu Serikali”.
“Meneja wa mkoa najua utasimamia barabara hii,” ipo miradi huwa inafeli kwa kutosimamiwa na fedha kutumika tofauti , sitegemei kuona fedha zinatumika tofauti na usanifu uliokwisha fanyika” alisema.
” Barabara hii ni muhimu, watu wanaitumia kwenda mbugani pamoja na kwenye bwawa la Mwalimu Nyerere, mpango wa Serikali ya awamu ya sita ni kukamilisha barabara hii kwa kiwango cha lami na hata ukienda kwenye ilani ya chama cha Mapinduzi ipo na inatakiwa kuijenga kwa kiwango Cha lami”alisisitiza Kasekenya.
Vilevile aliwaasa wananchi kulinda miundombinu ya barabara pamoja na madaraja pasipo kuihujumu ili iweze kudumu kwa kipindi kirefu.
Awali Meneja wa TANROADS mkoa wa Pwani ,Baraka Mwambage akielezea mradi wa Pugu – Manerumango km 60 na kutokea Pugu hadi Mloka urefu wa Km 157 ,alisema barabara ya Pugu-Manerumango imeshafanyiwa usanifu ,km 21 zimeshajengwa kwa kiwango cha lami na kipande kinachoendelea kujengwa sasa ni km 5.14.
“Ujenzi unaoendelea unaigharimu Serikali sh. Biln 7.88 na sehemu inayojengwa kwa sasa imeshafanyiwa usanifu, kutoka Pugu hadi Manerumango km 60 tayari zimeshafanyiwa usanifu” alisema Mwambage.
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Nickson Saimon aliipongeza Serikali kwa ujenzi wa barabara hiyo ,pia alimshukuru Naibu Waziri huyo kutembelea mradi huo, na kusema kulikuwa na changamoto ya fidia ambayo anamshukuru TANROADS mkoa wa Pwani inashughulikia .