……………………………….
Na. Farida saidy, Morogoro
Chuo Kikuu cha Kilimo SUA kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha
Kilimo cha nchini China vimefanikiwa kuendesha mafunzo ya kilimo
cha kisasa na kibiashara yenye lengo la kusaidia teknolojia za mazao
kwa wakulima ili waweze kulima kwa tija.
Mafunzo hayo ya wiki mbili yaliyoandaliwa na chuo kikuu cha Kilimo
cha China na SUA kupitia wizara husika chini ya mradi wa kuongeza
tija kwenye zao la Mahindi yameshirikisha Maafisa ugani kutoka
Halmashauri na vijiji kutoka Mikoa ya Morogoro na Dodoma ambao
wanatarajiwa kuwa sehemu ya kuleta mabadiliko kwa wakulima
waliopo katika maeneo yao .
Akiongea wakati wa kufunga mafunzo hayo, Mhadhiri kutoka Chuo
Kikuu cha Kilimo cha nchini China Profesa Xi Xiu Li ambaye ndiye
alikuwa mgeni rasmi katika hafla ya kufunga mafunzo hayo pamoja na
kutoa pongezi kwa washiriki wa mradi huo amesema mafunzo hayo ni
nafasi muhimu ya kupiga hatua kimaendeleo hasa katika kilimo.
Amesema kufanya kazi kwa bidii, ubunifu na kuaminiana ndio sababu
kubwa ya kupiga hatua kimaendeleo kama ambavyo china imefanikiwa
kupiga hatua kubwa kimaendeleo mpaka kufikia kipindi hiki ambacho
raia wa nchi hiyo wanaazimisha miaka 70 tangu Taifa hilo kuwa
Jamhuri.
“kufanya kazi kwa bidii, ubunifu na kuaminiana ndio sababu kubwa za
kupiga hatua za kimaendeleo kama ilivyo China ambayo imepiga hatua
kubwa kimaendeleo kufikia siku ya leo ambayo wananchi wake
wanasherehekea miaka 70 tangu kuwa Jamhuri,” Alisema Profesa Li.
Ameongeza kuwa Serikali ya China itaendelea kushirikiana na
Watanzania katika kubadilishana mbinu mbalimbali za kimaendeleo
ikiwemo kutambulisha tekinolojia mpya katika nyanja mbalimbali
ikiwemo kilimo.
Katibu Tawala msaidizi sehemu ya Uchumi na uzalishaji mali kutoka
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Rozalia Rwegasira
amewataka mafisa ugani waliohudhuria mafunzo hayo kuyatumia
ipasavyo ili iwe sababu ya kutatua changamoto zinazowakabili
wakulima katika maeneo ya vijijini.
Amesema wakulima wengi wanashindwa kutumia raslimali zilizopo
kuzalisha mazao mengi kutokana na weledi mdogo wa namna ya kulima
kilimo chenye tija.
Kwa upande wake Profesa Deogratias Rutatola ambae ni Mhadhiri
kutoka Chuo Kikuu cha kilimo SUA amesema kukamilika kwa mafunzo
hayo kunafunga njia kwa washiriki kufanya kwa vitendo yale yote
waliyojifunza katika kipindi chote cha wiki mbili.
Ameongeza kuwa ni wajibu wa maafisa ugani kuhakikisha
wanawaelekeza kwa ufasaha wakulima waliopo katika maeneo yao
namna bora ya kutumia eneo ambalo wanaweza kulimudu na kupata
mavuno makubwa kupitia teknolojia ya kisasa.
Mradi wa kuongeza tija kwenye zao la Mahindi ulinza tangu mwaka
2011 katika Wilaya za Kilosa, Gairo, Mvomero, Ulanga, Malinyi na
Kilombero na baada ya kuwa na mafanikio katika maeneo hayo
ziliongezeka wilaya nyingine kutoka mikoa ya Morogoro na Dodoma
lengo likiwa ni kuzalisha zao la Mahindi kwa kutumia teknolojia rahisi
na kufuata mbinu bora za kilimo.