Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Moshi Stadi kimepongezwa kwa kuwa na utaratibu wa kutoa mafunzo yanayowaunganisha wanafunzi moja kwa moja na shughuli halisi za Uzalishaji.
Pongezi zimetolewa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Adolf Mkenda Januari 10, 2023 alipotembelea Chuo hicho ili kuina namna mafunzo yanavyotolewa ambapo alipata fursa ya kutembelea karakana mbalimbali zilizopo chuoni hapo na kuongea na wanafunzi pamoja na wakufunzi.
Prof. Mkenda amesema chuo hicho kimekuwa na utaratibu mzuri wa kuwawezesha wanafunzi kujifunza chuoni na baadaye kwenda kwenye makampuni ama mashirika mbalimbali kufanya mafunzo kwa vitendo jambo ambalo linawajengea umahiri.
“Ushirikiano wa VETA Kilimanjaro na makampuni kama ya madini ni wa kupongezwa nimeona wameleta vifaa hapa kwa ajili ya kufundishia na kujifunzia, hii ni taratibu tunapenda isambae na kwa vyuo vingine” amesema Prof Mkenda.
Waziri huyo ameongeza kuwa kuna makampuni ambayo yanatoka nje yanakuja kufanya shughuli zake nchini wangependa kuona vijana wanapata mafunzo na ujuzi ambao yatawawezesha kuwatumia katika shughuli zao.
Amewataka VETA kuweka dirisha ambalo litawaeleza kama wanataka wataalam waliopitia VETA wanawatoa wapi ama hata kuwauliza ni aina gani ya mafunzo ambayo wanataka yatolewe kwa vijana wanaotaka kuwaajiri.
Ameongeza kuwa mafunzo yanayotolewa yanalenga kuona wanafunzi wanaweza kuyamudu mazingira ya kazi pale walipo hapa nchini na hata nje ya Nchi.
Aidha, Prof. Mkenda amesema Serikali inafanya tracer study ya watu waliopitia VETA ili kujua wapo wapi, wameajiriwa na nani au wamejiajiri wenyewe na je waliowaajiri wanasemaje kuhusu tathimini ya utendaji wao, kama wamejiajiri kujua mafunzo waliyopata VETA yanamuwezesha kutekeleza kazi kwa umahiri na pia watoe ushauri juu ya maboresho ya mafunzo.