**************************
Na John Walter-Babati
Mkuu wa Mkoa wa Manyara Charles Makongoro Nyerere amesema katika mkoa huo wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza wataingia darasani bila usumbufu wowote kwa kuwa serikali imejenga madarasa ya kutosha.
Nyerere amesema hayo leo Januari 10, 2023 wakati wa ziara yake ya ukaguzi wa ujenzi wa Madarasa shule ya Sekondari ya kutwa Magugu na shule mpya ya Sekondari Sarame kata ya Mgugu wilaya ya Babati.
Amesema milioni 40 za tozo zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan zimejenga madarasa mawili shule ya Magugu na Milioni 470 zimejenga shule mpya ya Sekondari Sarame kupunguza makali ya wanafunzi kwenda umbali mrefu.
Aidha ameipongeza Halmashauri ya wilaya ya Babati kwa kufanya vizuri katika ujenzi wa Madarasa hayo ya Mama Samia Suluhu Hassan.
Nyerere amewataka wazazi wenye watoto wanaopaswa kuingia kidato cha kwanza mwaka 2023 kuwapelekea shule bila kujali hali walizo nazo kwa kuwa lengo la serikali ni kuhakikisha kila mtoto anapata elimu.
Naye Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Babati Anna Mbogo amesema watahakikisha kila mwanafunzi aliyechaguliwa kujiunga na elimu ya Sekondari anapokelewa shuleni.
Amesema Halmashauri ya wilaya ya Babati kupitia fedha zilizotolewa na Rais Dr. Samia Suluhu Hassan (KAPU LA MAMA) wamejenga madarasa 20 na yote yamekamilika yakiwa na madawati 50 kwa kila darasa.
Utakumbuka kuwa Serikali imeondoa ada elimu ya msingi hadi kidato cha sita ili kuongeza uwezekano wa watanzania wengi kupata elimu kwa ufasaha mkubwa.
Mwenyekiti wa Kijiji Cha Magugu Deoglas Ngalawa amemuomba mkuu wa mkoa wa Manyara kujenga barabara kwenda shule ya Sarame.