*****************
Na. WAF – Dodoma
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Prof. Abel Makubi amesema jukumu la utoaji wa Elimu ya Muswada wa Bima ya Afya kwa Wote sio suala la Wizara ya Afya peke yake bali ni kwa kila kiongozi na Mwananchi.
Prof. Makubi ameyasema hayo leo kwenye kikao na wakuu wa vitengo vya Habari na Mawasiliano pamoja na Maafisa Habari wa Taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Afya kwenye kikao kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Wizara Jijini Dodoma.
“Katika kuweka mikakati ya Uelimishaji jamii juu ya Muswada wa elimu ya Bima ya Afya kwa Wote kabla ya kujadiliwa Bungeni mwishoni mwa Mwezi Januari, 2023 inatupasa tutoe elimu kwa kushirikiana na sekta nyingine kama tulivyofanya kwenye Sensa na UVIKO-19.” Amesema Prof. Makubi
Amesisitiza pia, ni muhimu kuzungumzia umuhimu na faida za kujiunga na Bima ya Afya kwa wote pindi itakapopitishwa na Bunge ili wananchi waweze kuelewa vizuri na kujiunga.
Aidha, Prof. Makubi amewakumbusha pia Maafisa hao wa Habari wa Taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Afya pamoja na watoa huduma mbalimbali za Afya kuwa lengo la Serikali kupitia Wizara ya Afya ni utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Hivyo, amewataka watoa huduma za Afya wote nchini kuzingatia utoaji wa huduma bora kwa kufuata miongozo na sheria zilizopo nchini.