Wafuasi wa jukwaa la Mtandao wa kijamii wa Whatsapp lijulikanalo kama KAGERA MPYA wamefika katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera Bukoba kwa lengo la kutoa msaada wa vitu mbalimbali kwa wagonjwa waliolazwa hospitalini hapo.
Akiongea kwa niaba ya wanajukwaa wenzake Shaban Rashid ambaye ni diwani kata Bakoba ameeleza kuwa waliamua kufanya jambo hilo la kuigusa jamii wanayoishi nayo ambayo kwa namna moja imekuwa ikishindwa kupata mahitaji muhimu wawapo hospitalini.
Amesema kuwa wazo la kutoa misaada hiyo lilitokana na wanajukwaa wenyewe kuamua kumshukuru Mungu kwa kuwavusha salama mwaka 2022 na kuona ipo haja ya kutoa shukrani zao kwa kutoa walichojaaliwa kwa wagonjwa ambao pengine mwaka huu umewakuta wakiwa wanaumwa.
Amesema kuwa vitu walivyoleta ni sabuni, sukari, pampasi na maziwa ya kopo ambavyo vitu hivyo vitaweza kuwasaidia wagonjwa hao na kuwarejeshea tabasamu.
Dkt Asheli ni Katibu wa Hospital hiyo, ametoa shukrani zake za dhati kwa wanajukwaa hilo kwa kuona umuhimu wa kutoa michango yao na kuwaletea wale wenye uhitaji ambao wamekuwa wakihangaika na baadhi ya mahitaji yao.
Dkt. Asheli ameitaka jamii kuendelea kujitoa na kuiga mfano mzuri ulioanzishwa na jukwaa la KAGERA MPYA, kwakuwa wahitaji bado ni wengi na kuongeza kuwa wamekuwa wakiwapokea wagonjwa mbalimbali ambao hawana ndugu wala jamaa hivyo misaada hiyo itaweza kuwasaidia.
Katika hatua nyingine wanajukwaa hao wameishukuru serikali ya wamu ya sita chini ya Dkt. Samia Suluhu Hasani kwa kuendelea kuboresha huduma za afya katika mkoa wa Kagera sambamba na upanuzi wa hoospitali ya Rufaa ya mkoa wa Kagera Bukoba ambapo ujenzi wa majengo mbalimbali unaendelea ikiwemo nyumba ya mtumishi.
Wameeleza kuwa utaratibu huu wa kuchangia huduma za kijamii utakuwa endelevu kwani wamekuwa wakiguswa na masuala ya kijamii ambapo wameongeza kuwa kabla ya kufika hospitalini hapo walianza na matembezi kwaajili ya kuweka miili Yao Sawa na jambo hilo watakutwa wanalifanya kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi.