*********************
Na John Walter-Manyara
Wananchi wameaswa kuendelea kuiombea amani ya nchi ili iendelea kuwa mfano wa kuigwa katika kutunza na kuilinda amani iliyopo.
Wito huo umetolewa na mbunge wa jimbo la Mbulu Mjini mkoani Manyara Zakaria Paul Issay wakati akitoa salamu za mwaka mpya mara baada ya kushiriki misa takatifu ya mkesha wa Krismass katika Parokia ya Sanu.
Amesema kuwa Tanzania imeendelea kuwa na amani kutokana na sala maombi yanayofanywa na watu waliojitoa kwa ajili ya kuliombea taifa.
Isaay amewaomba Wananchi pia kuwaombea viongozi ili waendelee kufanya kazi kwa uadilifu.
Kuhusu hali ya uchumi, amesema kuwa hali iliyopo kwa sasa siyo Tanzania peke yake na kwamba huenda imesababishwa na kutokuwa na amani ikiwemo vita vya Urusi na Ukreini.
Amesema kadri vita inavyoelendelea baadhi ya bidhaa na huduma zinapungua katika soko la dunia na hivyo Tanzania nayo inaathiriwa na vita hivyo.
Kutokana na athari hizo ameendelea kutoa wito wa kuendelea kuomba ili Mungu aondoe balaa hilo la vita, pamoja na ukame ambao umeathiri maeneo mbalimbali ya dunia.
katika salamu zake alizozitoa kwa niaba ya serikali Wilayani Mbulu Mbunge Issay amewatakia wote heri ya mwaka mpya 2023, huku akimuomba Mungu aendelee kuwajalia afya njema ili wazidi kuchapa kazi.