*********************
Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
MKUU wa mkoa wa Pwani, alhaj Abubakari Kunenge amezitaka Halmashauri na Taasisi za Serikali kuhakikisha zinaongeza mapato pamoja na kuibua vyanzo vipya vya mapato ili kuinua uchumi wa Mkoa.
Aidha ameyataka mabaraza ya madiwani kuzungumza uchumi na fursa zilizopo ili kwenda na kipaombele cha kuinua uchumi .
Akizungumza katika kikao Cha Ushauri Cha mkoa (RCC) Kunenge alieleza ,wote kwa umoja wazungumzie mapato ili kupunguza kukopa, kwani mkoa huo ni wa viwanda haiwezekani kuona unashuka kiuchumi.
“Halmashauri ziongeze mapato, tuende pamojaa na uwezo wa kiuchumi, na niseme hapo nikizungumzia mapato sio halmashauri tuu na Taasisi zetu za Serikali zihakikishe zinaongeza mapato,hata Kama mnakusanya ,mtuambie mnakisanya kiasi gani na malengo yenu ni yapi”alifafanua Kunenge.
Hata hivyo Kunenge aliwapongeza watendaji wote kimkoa kwa kufanya kazi timu moja ,na kuongeza kusema ni wajibu wa kila mmoja kufanana na mahitaji ya nafasi aliyonayo .
Nae Ofisa Mipango na Uratibu Mkoani Pwani,Rukia Muwango alieleza ,mwaka wa fedha 2022/2023 mkoa huo umeidhinisha bajeti ya zaidi ya sh.bilioni 335.1 kati ya hizo ruzuku ya matumizi ya kawaida ni bilioni 206.063.8 ,sh.bilioni 80,5 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na bilioni 48,4 za mapato ya ndani ya Halmashauri.
Alieleza bajeti ya mkoa wa Pwani kwa mwaka 2022/2023 imeongezeka kwa Bilioni 36,279,573,000 sawa na asilimia 12.14 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka 2021/2022.
Rukia alifafanua , ongezeko hilo linatokana na ongezeko la mishahara kwa asilimia 19.38, matumizi mengine (oc) asilimia 21.82, fedha za ndani kwa ajili ya miradi ya maendeleo asilimia 9.44 na mapato ya ndani ya Halmashauri asilimia 23.33.
“Bajeti ya miradi ya maendeleo kwa fedha za nje imepungua kwa asilimia 24.86 ,kwa ujumla bajeti ya mkoa imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka.
Kuhusu changamoto, Rukia alisema mkoa umepata changamoto kubwa ya kufanya uhamisho wa ndani na nje wa bajeti kwa fedha zilizopokelewa nje ya bajeti.
Rukia alifafanua , changamoto hii imesababisha ucheleweshaji katika utekelezaji wa shughuli zilizokusudiwa.
Kufuatia hali hiyo, mkoa utawasilisha maombi ya kuwekewa ukomo wa bajeti kwenye bajeti ya mwaka 2023/2024 ili kuondoa changamoto ya matumizi ya fedha zilizotolewa na wadau wa maendeleo.