Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
SERIKALI Mkoani Pwani,imelikabidhi Jukwaa la uwezeshaji wanawake kiuchumi Kampuni Ya GoMAMA yenye mtaji na hisa ya Bilioni 50.
Akitoa rai wakati wa makabidhiano ya majukumu ya Kampuni ya wanawake ya GoMAMA (PLC) kupitia Jukwaa la uwezeshaji wanawake kiuchumi Mkoani Pwani,yaliyofanyika Kibaha , Katibu Tawala mkoa wa Pwani,Zuwena Omari alilitaka Jukwaa hilo ,lihamasishe wanawake kuanzia ngazi ya chini ya Vijiji kujiunga na jukwaa pamoja na vikundi ili waweze kunufaika na fursa mbalimbali zinazopatikana kwa ajili ya kujiinua kiuchumi.
Aidha alilitaka jukwaa hilo kuanzisha majukwaa mapya katika maeneo ambayo bado hayajaundwa sanjali na kubuni miradi ya uzalishaji .
Zuwena alieleza,Ni wakati wa wanawake wa vijiji, vitongoji nao kujiona ni sehemu ya fursa zinazojitokeza kumkomboa mwanamke kiuchumi.
Hata hivyo alieleza kwasasa yapo majukwaa yaliyosajiliwa 945 Mkoani hapo ,wajumbe zaidi ya 28,000 ikiwa ni sawa na asilimia 54 .
“Serikali itakuwepo kama ilivyo katika Taasisi nyingine,tutaendelea kuwa washauri kuhakikisha Kampuni inaendelea kung’ara ,sisi Serikali wakati tunashiriki hili suala tulitaka kuona wanawake kwenye vikundi vikiimarika kiuchumi ,nawasihi mkawahamasishe na wenzetu wa chini kujiunga tuone nao wakibadilika kiuchumi na waone ni sehemu ya fursa hizi”
“Kama tumesajili kupata Kampuni hitaji la wanawake kuona wanapiga hatua,asilimia 60 ya umiliki na hisa upo katika majukwaa ya wanawake,hivyo Hawa wenzetu wa hali ya chini tusiwaache nyuma , wanaweza kujiona sio sehemu ya hisa hizi”
Pia Zuwena aliwataka viongozi wa Jukwaa hilo kwenda kutoa elimu ya umuhimu wa Kampuni ya GoMama ,Lengo lake ili wanawake wengi waweze kunufaika.
Akiwasilisha taarifa ya makabidhiano ya uendeshaji wa Kampuni ya GoMama mtaalam mshiriki aliyeratibu mchakato wa uanzishaji Kampuni ya GoMama Mkoani Pwani ,Dr.Ramadhani Mwaiganju alieleza mtaji na hisa ni Bilioni 50.
Alisema ,kila hisa ina thamani ya sh.1,000 ambapo Kampuni itaendeshwa na bodi ya wakurugenzi na kuidhinishwa na mkutano Mkuu.
“Asilimia 60 ya hisa wahamasishwe ziende kwa wanawake wa majukwaa huku asilimia 40 wanahamasishwa wananchi kutoka maeneo mbalimbali nchini wakiwemo wanaume”alifafanua Mwaiganju.
Mwaiganju alitaja malengo ya kampuni kuwa ni kuanzisha biashara zitakazosaidia wanawake kiuchumi na wakala wa kuuza vifungashio kutoka nje ya nchi.
Akishukuru Mwenyekiti wa Jukwaa la Uwekeshaji Kiuchumi Mkoani Pwani,Mariam Ulega alisema safari haikuwa rahisi na ameshukuru kufikia hatua ya kukabidhiwa Kampuni ya GoMama.
“Namshukuru mh.Rais Samia Suluhu Hassan kwani yeye ndio muanzilishi wa majukwaa haya, sisi Kama Jukwaa tunataka tuje na mbinu ya kupiga hatua kwa kwenda na Kasi ya mh Rais kwani tumeona akifanya kazi kubwa ya kuifungua nchi ,na sisi tushapewa dira ,nafasi kwa kukabidhiwa kampunii hii ,Tutahakikisha tunatoa elimu ,tutafanya kazi bila kulala”
“Mimi kama Mwenyekiti nitahakikisha Kampuni inasonga mbele ili kumuunga mkono mh.Rais kuhakikisha mwanamke anainuka kiuchumi”alibainisha Mariam.