Tenki lenye uwezo wa kuhifadhi lita 90,000 za maji lililoanza kuhudumia wakazi wa kijiji cha Nyalailembo wilyani Mbeya.
Msimamizi wa ujenzi wa mradi wa maji Shizuvi Halmashauri ya Mbeya Mhandisi Felix Msangi,akiwaonesha baadhi ya wakazi wa kijiji cha Nyalailembo tenki la maji lililojengwa kupitia fedha za mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Uvico-19.
Afisa Utumishi wa wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)mkoa wa Mbeya Emile Mpasi kulia,akizungumza na baadhi ya wazee wa kijiji chaNyalailembo wilayani Mbeya baada ya kukabidhi rasmi mradi wa maji wa Shizuvi utakaohudumia zaidi ya wakazi 2,474 wa kijiji hicho.
Baadhi ya akina mama wa kijiji cha Nyalailembo Halmashauri ya wilaya Mbeya mkoani Mbeya wakichota maji katika moja ya vituo vya kuchotea maji kilichojengwa kupitia mradi wa maji wa Shizuvi.
Msimamizi wa mradi wa maji wa Shizuvi Mhandisi Felix Msangi kulia na Afisa Utumishi wa Ruwasa mkoa wa Mbeya Emile Mpasi katikati,wakimtua ndoo ya maji mkazi wa kijiji cha Nyalailembo kata ya Shizuvi wilayani Mbeya Jane Mwashibanda.
Baadhi ya akina mama wa kijiji cha Nyalailembo kata ya Shizuvi wilayani Mbeya,wakimsikiliza afisa utumishi wa Ruwasa mkoa wa Mbeya Emile Mpasi kulia baada ya kutembelea mradi wa maji Shizuvi uliotekelezw na Ruwasa kwa gharama ya Sh,milioni 482,kushoto ni msimamizi wa mradi huo Mhandisi Felix Msangi.
………………………..
Na Muhidin Amri,Mbeya
UJENZI wa mradi wa maji Shizuvi kijiji cha NyalaIlembo Halmashauri ya wilaya Mbeya mkoani Mbeya uliotekelezwa na wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa),umekamilika kwa asilimia 100 na hivyo kumaliza kabisa kero ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama iliyokuwepo kwa wakazi wa kijiji hicho kabla na baada ya Uhuru.
Mradi huo umetekelezwa kwa gharama ya Sh.milioni 482 kupitia fedha za mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ugonjwa wa Uvico-19, utahudumia takribani wakazi 2,474.
Msimamizi wa mradi huo Mhandisi Felix Msangi alisema,mradi wa maji wa Shizuvi ni miongoni mwa miradi sita iliyotekelezwa na wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa) kwenye majimbo sita mkoani Mbeya.
Alitaja kazi zilizofanyika ni kujenga dakio la maji(Intake) kujenga tenki la lita 90,000,kulaza mabomba urefu wa km 16.5 na kujenga vituo 16 vya kuchotea maji kwenye makazi ya wananchi.
Aidha alisema,mradi wa maji InyalaIlembo umemaliza/kuondoa kero ya muda mrefu ya huduma ya maji safi na salama,hivyo kuwezesha wananchi wa kijiji hicho na maeneo jirani kupata muda mwingi wa kushiriki vyema shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
Alisema wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa),unaendelea kutekeleza miradi ya maji katika vijiji mbalimbali mkoani Mbeya na kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama wakati wote na wanatumia maji kufanya shughuli zao za kiuchumi kwa urahisi.
Kwa upande wake Afisa Utumishi wa Ruwasa mkoa wa Mbeya Emile Mpasi,amewaasa wakazi wa kijiji hicho kuhakikisha wanatunza vyanzo vya maji,na kulinda miundombinu ili mradi huo uweze kudumu kwa mrefu na kuwaondolea kero ya huduma ya maji safi na salama katika maeneo yao.
Alisema serikali imetumia fedha nyingi kujenga mradi huo,hivyo kilichobaki ni kwa wananchi ambao ndiyo wanufaika kuhakikisha hakuna uharibifu wa miundombinu na vyanzo vya maji na kutumia mradi huo kufanya shughuli mbalimbali za uzalishaji mali.
“mradi huu ni muhimu sana kwani utawezesha na kurahisisha shughuli za kiuchumi kufanyika,hizi ni jitihada za serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na mama yetu Rais Dk Samia Suluhu Hassan ambaye ametafuta fedha kwa ajili ya kutatua changamoto ya maji kwa wananchi wa kijiji hiki”alisema Mpasi.
Amewataka viongozi wa chombo cha watoa huduma ya maji ngazi ya jamii(CBWSO),kuhamasisha wananchi kuingiza maji ndani ya nyumba zao na kuweka bei rafiki pindi wananchi watakapoanza kulipia gharama ya maji kwenye vituo(DP)na watakaohitaji kuingiza huduma hiyo majumbani.
Naye mwenyekiti wa chombo cha watoa huduma ya maji ngazi ya jamii (CBWSO) kijiji cha Nyalailembo Joshua Mwandete alisema,kabla ya kujengwa kwa mradi huo wananchi hasa wanawake na watoto walitembea kati ya Dk 40 hadi 60 kwenda kuchota maji kwenye mito na mabonde.
Mwandete alisema,baada ya kukamilika kwa ujenzi wa mradi mateso yamemalizika na maisha ya wananchi yamebadilika kwani sasa wanatumia fursa ya uwepo wa maji ya bomba kufanya shughuli za maendeleo ikiwamo ufugaji,ujenzi wa nyumba bora na kilimo cha bustani.
Alisema,watatumia CBWSO hiyo kuboresha upatikanaji wa huduma huduma ya maji kwa wananchi na kusambaza mtandao kwenye maeneo yasiofikiwa na huduma ya maji ili kila mmoja aweze kufikiwa na kupata maji safi na salama katika makazi yake.
Baadhi ya wananchi wa kijiji hicho,wameipongeza serikali kupitia wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)kujenga mradi huo ambao umesaidia kumaliza kero ya upatikanaji wa huduma ya maji.
John Mwainga alisema,licha ya mradi huo kukamilika kwa asilimia 100,lakini bado kuna vijiji viwili ambavyo bado havijapelekewa maji na kuiomba Ruwasa kupeleka mtandao wa maji katika vijiji hivyo.
Sistery Mwakalebela mkazi wa kitongoji cha Tunduma,amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kutoa fedha kwa ajili ya kutekeleza mradi wa maji ambao umemaliza mateso ya muda mrefu kwa wanawake ambao walilazimika kutumia muda mwingi na kutembea umbali mrefu kwenda kutafuta maji.