*******************
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mbunge wa Mbeya Mjini, Mhe. Dkt. Tulia Ackson leo Januari 2, 2023 amewaongoza Wananchi wa Kata ya Ruanda Jijini humo katika zoezi la kufanya usafi katika eneo la Umati ambalo limekithiri uchafu kwa muda mrefu.
Dkt. Tulia amesikitishwa na mlundikano wa taka ambazo hazijazolewa kwa muda mrefu huku akiwataka Wananchi wa Kata hiyo pamoja na Jiji hilo kwa ujumla kuzingatia usafi katika maeneo yao ili kusaidia kulinda hadhi ya Jiji.
Aidha Dkt. Tulia amechukua fursa hiyo kuwaeleza Wananchi hao kuhusu utaratibu mpya wa Jiji wa kuondoa maghuba katika mitaa na zoezi la uzoaji taka kuelekezwa katika Kata husika.
Mwenyekiti wa mtaa wa Benki, Anna Ndimbwa amesema mara kadhaa amefuatilia uzoaji wa taka katika eneo hilo bila mafanikio licha ya taarifa kuziwasilisha kwa Diwani wa Kata ya Ruanda Reuben Kipalule.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Ruanda, Reuben Kipalule amekiri mzabuni kushindwa kuzoa taka kwa wakati na kuahidi kuongeza mzabuni mwingine ili kumudu uzoaji wa taka katika Kata yake.
Naye Kaimu Mstahiki Meya wa Jiji la Mbeya, Kefasi Changani Mwasote amekiri kuwepo kwa uchafu katika Kata nyingi na kuahidi kulisimamia zoezi la usafi ili Jiji liwe safi.
Amesema katika vikao vya Baraza waliazimia zoezi la usafi lisimamiwe na wazabuni kupitia vikundi mbalimbali na kuyaondosha maghuba katika maeneo yote ili taka zizolewe kwa muda maalumu kila kata kwa namna watakavyokubaliana.
Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya Wakili Trifonia Kisiga amesema watashirikiana na Madiwani katika kila Kata ili kuhakikisha Jiji linakuwa na mazingira safi.
Hata hivyo amesema utaratibu mpya umepunguza gharama za uendeshaji kwa Jiji kwani shughuli zote za makusanyo hufanyika katika kila Kata.
Afisa mazingira Jiji la Mbeya, Nimrod Kiporoza ameagizwa na Spika Dkt. Tulia Ackson kuondoka ofisini badala yake apite katika kila kata kubaini changamoto za kuwepo mlundikano wa taka.
Hili ni zoezi la pili kufanywa na Spika Dkt. Tulia hasa maeneo yaliyoyokithiri kwa uchafu ambapo hivi karibuni alisimamia zoezi la usafi katika eneo la Soko la Sido Kata ya Iyela ambako pia wafanyabiashara walilalamika kutozolewa taka kwa muda mrefu.