Na Hellen Mtereko, Mwanza
Polisi jamii,vikundi vya sungusungu,wenyeviti wa vijiji na watendaji wa Kata wametakiwa kufuata taratibu na kanuni za nchi katika kutekeleza majukumu yao hasa kwenye upande wa ulinzi na usalama hatua itakayosaidia kupunguza uhalifu au kumaliza kabisa hapa nchini.
Wito huo ulitolewa jana Ijumaa Disemba 30, 2022 na Inspekta Jovita Tibangayuka kutoka Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza ambae ni Mkaguzi wa kata ya Nyamizeze iliyoko katika Wilaya ya Sengerema Mkoani hapa wakati akitoa elimu kwa viongozi hao.
Alisema elimu hiyo ililenga kuwaelimisha juu ya ukamataji salama,kuimarisha ulinzi,kuwafundisha mambo mbalimbali ya ulinzi na usalama ambayo yatasaidia kukomesha uhalifu katika kata ya Nyamizeze na Wilaya ya Sengerema kwa ujumla.
Tibangayuka alisema uhalifu ukizuiwa kuanzia ngazi ya familia Taifa litaondokana na changamoto hiyo na Maendeleo yatapatikana kwani watu watafanya kazi zao kwa usalama na amani.
Alisema kwa upande wa Polisi jamii uelewa ulikuwa mdogo wa kutekeleza majukumu yao kwani waliamini kumkamata mtu hadi wampige lakini kutokana na elimu waliyoipata anaamini watafanya kazi zao kwa weledi.
Kwa upande wao viongozi waliopatiwa elimu walisema wanalishukuru Jeshi la Polisi kwa kuwapelekea Mkaguzi kwenye Kata yao huku wakiahidi kumpa ushirikiano.
Walisema elimu waliyoipata itawasaidia kufanya kazi zao kwa weledi na ufanisi mkubwa.