Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji madini Mkoa wa Manyara MAREMA, Justin Nyari (kushoto) akiwa na Rais wa shirikisho la vyama vya wachimbaji madini Tanzania FEMATA John Bina.
………………………..
Na Mwandishi wetu, Mirerani
MWENYEKITI wa chama cha wachimbaji madini Mkoa wa Manyara (MAREMA) Justin Nyari amesema wachimbaji wa madini ya Tanzanite wa Mji mdogo wa Mirerani, Wilayani Simanjiro, hawatoroshi madini hayo.
Nyari amesema wachimbaji madini ya Tanzanite wakishapata uzalishaji wanafika nayo ndani ya ukuta na kufanyiwa tathimini kisha taratibu nyingine za uuzaji hufuata na siyo vinginevyo.
Amesema hata hivyo Serikali imejenga ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite, hivyo kuwa vigumu wachimbaji madini hayo kutoroka nayo kutokana na ulinzi huo.
“Pamoja na wafanyakazi wa Wizara ya Madini pia kuna ulinzi mkubwa wa vyombo vya ulinzi na usalama ndani ya ukuta huo na upekuzi huwa unafanyika hivyo siyo rahisi wachimbaji kutorosha madini hayo,” amesema Nyari.
Mchimbaji wa madini ya Tanzanite, Sokota Mbuya amesema kuwa ni upotoshaji mkubwa kuwasema wachimbaji wa Tanzanite wanayatorosha madini hayo.
“Mchimbaji hawezi kutorosha madini kwenye ukuta wenye jeshi la wananchi, usalama wa Taifa, polisi, uhamiaji na TAKUKURU,,” amesema Sokota.