********************
Na Mwamvua Mwinyi, Rufiji
SERIKALI Mkoani Pwani,imewaasa wananchi wa kata ya Chemchem ,Utete wilayani Rufiji Mkoani Pwani kupeana ushirikiano pamoja na mwekezaji wa mradi mkubwa wa uzalishaji Sukari Lake Agro sugar estates ,ambae anatarajia kutoa ajira zaidi ya 3,000 na kugharimu dollar za kimarekani milioni 321 ifikapo 2025.
Akitembelea na kukagua eneo la mradi huo, mkuu wa mkoa wa Pwani ,alhaj Abubakari Kunenge alieleza ,kwa upande wa Serikali imembariki mwekezaji huyo kuendelea na mchakato ya uwekezaji kwa manufaa chanya ya kata , wilaya, mkoa na Taifa kijumla.
Alieleza, kiwanda hicho kinakwenda kutatua uhaba wa sukari na kuondokana na uingizaji wa bidhaa hiyo kutoka nje ya nchi.
Kunenge alieleza, kwasasa mahitaji ya sukari (brown sugar) ni tani 440,000 na sukari nyeupe ya Viwandani tani 220,000 , hivyo uwekezaji huo ni mkombozi kwa wanaRufiji.
“WanaRufiji tunafungua mkoa, wilaya,wapo wenzenu wanalilia wawekezaji,ni wajibu wetu kuhakikisha tunatoa ushirikiano,Panapokuwa na misuguano hakuna maendeleo,elimu izidi kutolewa jamii ielewe umuhimu wa mradi huu badala ya kuweka vikwazo”
“Huwezi kupata tija kwa kuvutana ,mivutano haina manufaa, kwani mradi unahitaji wananchi na wananchi wanahitaji mradi,unapochelewa mradi mnaongeza gharama za mradi kwa mwekezaji na kumpa hasara”alifafanua Kunenge.
Hata hivyo Kunenge alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa matokeo makubwa ya kazi yake inayoonekana kufanyika katika mkoa huo ikiwemo katika uwekezaji,miradi mikubwa ya kimkakati, maji,umeme, miundombinu,elimu na afya
Aidha Kunenge alieleza ni wajibu wa wazazi na walezi Rufiji Mkoani Pwani kuandaa vijana wao ili waje kunufaika na mradi huu.
“Nimetembelea viwanda 28 kila nilipopita wawekezaji watoa changamoto ya vijana wazawa kushindwa kuendelea na kazi ,suala ambalo linasikitisha “alibainisha Kunenge.
Nae Meneja uwekezaji Lake Agro, Abubakari Nassoro alieleza ,wameanza Septemba mwaka 2021 ,ambapo wapo kwenye hatua ya maandalizi ya vitalu miche ya miwa,wamechimba bwawa la maji linalobeba ujazo wa Lita milioni 4.8,umeme na kuboresha miundombinu mbalimbali.
Alieleza, kiwanda cha sukari kinatarajia kuanza mwaka 2025 kwa kuzalisha tani 300,000 za sukari na pia watatumia kilimo cha mkataba kwa wakulima wa nje.
Nassoro alieleza ,eneo la uwekezaji ni hekta 15,000 ambalo awamu ya kwanza wamefanya tathmini na kulipa fidia kwa Wananchi 42 kiasi cha sh.milioni 172 huku awamu ya pili wanatarajia kuwalipa fidia wananchi 130 na Sasa wapo katika hatua ya kusubiri muongozo wa Serikali.