Kikosi cha wachezaji 22, viongozi pamoja na benchi la ufundi wataondoka Jijini Dar es salaam kesho kuelekea Mbarali mkoani Mbeya kwenye mchezo wa Ligi kuu ya NBC Soka Tanzania bara dhidi ya Ihefu utakaopigwa Januari tatu katika uwanja wa Highland Estates mkoani humo.
Kikosi hicho cha wana Kino Boys chini ya kaimu kocha Mkuu Hamad Ally kitaonda Jijini Dar es Salaam ikiwa ni mara baada ya kukamilisha maandalizi ya mchezo huo tangu iliporejea kutoka Jijini Mwanza Disemba 27.
Aidha katika mchezo huo Timu hiyo ya Manispaa ya Kinondoni itakuwa ugenini Januri tatu na kwamba kama Timu imejipanga kukabiliana na wapinzani hao ambao kwa hivi sasa wamekuwa na matokeo mazuri kwenye uwanja wao wanyumbani .
“Tumetoka kupoteza mchezo wetu dhidi ya Simba siku ya Disemba 26 lakini bado tupo kwenye hari na morali nzuri kwa sababu ni sehemu ya matokeo kwenye mpira wa miguu, hatupaswi kurudi nyuma badala yake tumejikita zaidi kusonga mbele kwenye michezo iliyopo mbele yetu hivi sasa.
“Tunapokwenda Mbarali tunafahamu fika kuwa tutakuwa na mchezo mgumu na wenye ushindani kutokana na kwamba Ihefu wamekuwa na wakati mzuri kwenye matokeo, na kwamba kama Manispaa ya Kinondoni tumejiandaa vya kutosha ilikuhakikisha kwamba alama tatu muhimu zinapatikana.
Kwa upande wa Afya za wachezaji, wote wapo kwenye hali nzuri na kwamba bado KMC FC itaendelea kukosa huduma za wachezaji wake muhimu wawili ambao ni Hance Masoud Msonga pamoja na Emmanuel Mvuyekure ambao bado wanaendelea kupatiwa matibabu kutokana na majeraha waliyoyapata mwezi mmoja uliopita.
KMC FC inakwenda kwenye mchezo wa mzunguko wa 19 kabla ya kuanza kwa mapumziko ya kupisha michuano ya kombe la mapinduzi ikiwa kwenye nafasi ya tisa, huku ikicheza jumla ya michezo 18 na kukusa alama 22 katika msimamo wa Ligi Kuu ya NBC Soka Tanzania bara.