*******
Na Englibert Kayombo, WAF – Dar Es Salaam.
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amepiga marufuku ya kuendelea na ujenzi wa majengo mapya katika Hospitali zote za Rufaa za Mikoa nchini ambazo hazina mpango wa uendelezaji ardhi (Masterplan)
Waziri Ummy ametoa agizo hilo leo alipofanya ziara ya kushtukiza katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwananyamala Jijini Dar Es Salaam na kukuta ujenzi wa majengo ukiendelea ambayo hayajawekwa kwenye mpangilio mzurii wa kutoa huduma zinazoendana pindi yatakapo kamilika.
“Nimepiga marufuku hapa Mwananyamala, hatutoweka jengo lolote bila ya kuwa na ‘Masterplan’ ya Hospitali, tukiwa na ‘Masterplan’ huduma pia zitakuwa zinaendana na zinapatikana kwa ukaribu” amesema Waziri Ummy Mwalimu
Amesema kwa hali iliyopo sasa wananchi wanatumia muda mwingi na kuzunguka kufuata huduma ndani ya Hospitali kwakuwa majengo ya kutolea huduma yamewekwa mbali mbali.
“Unaenda Maabara unaikuta iko peke yake, vipimo vya Xray vipo peke yake, UltraSound iko peke yake, tunataka kama ni masuala ya uchunguzi mgonjwa anakwenda kwenye jengo moja anapata huduma zote za uchunguzi” amefafanua Waziri Ummy Mwalimu.
Waziri Ummy amesisitiza kuwa agizo hilo sio kwa ajili ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala bali ni la nchi nzima hususani kwa Hospitali zile za zamani ambazo zilijengwa bila ya kuwa na “Masterplan”