Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Dkt. Donald Wright akiwa kwenye picha ya pamoja na wahitimu wa mafunzo kwa wanawake wajasiriamali kutoka wilaya ya Bagamoyo na Mikoa wa Dar es salaam, mara baada ya kuhitimishwa kwa mafunzo hayo jana Desemba 21, 2022 katika ukumbi wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa)
Mratibu wa taasisi ya AWE, Dkt. Victoria Kisyombe akisikiliza kwa makini, hotuba ya Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Dkt. Donald Wright (hayupo pichani) katika hafla ya kufunga mafunzo ya wajasiriamali wanawake kutoka wilaya ya Bagamoyo na Mkoa wa Dar es salaam jana Desemba 21, 2022
Mmoja wa wahitimu wa mafunzo ya wajasiriamali wanawake akitoa maelezo ya namna anavyoanda bidhaa zake kwa Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Dkt. Donald Wright. Kulia kwa Balozi Wright ni mratibu wa taasisi ya AWE Dkt. Victoria Kisyombe
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Mhe.Nickson Simon akisalimiana na Balozi wa Marekani nchini Tanzania Dkt. Donald Wright wakati wa hafla ya kufunga mafunzo kwa wanawake wajasiriamali kutoka wilaya ya Bagamoyo na Mkoa wa Dar es salaam jana Desemba 21, 2022 katika ukumbi wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa)
Balozi wa Marekani nchini Tanzania Dkt. Donald Wright akitoa hotuba yake wakati wa hafla ya kufunga mafunzo kwa wanawake wajasiriamali kutoka wilaya ya Bagamoyo na Mkoa wa Dar es salaam jana Desemba 21, 2022 katika ukumbi wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa)
Mgeni rasmi katika hafla ya kufunga mafunzo kwa wanawake wajasiriamali kutoka wilaya ya Bagamoyo na Mkoa wa Dar es salaam ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Nickson Simon akitoa hotuba yake.
**************
Na Mwandishi Wetu
BALOZI wa Marekani hapa nchini Dkt. Donald Wright amesema, kuwajengea uwezo wa kiuchumi wanawake ndio njia ya haraka zaidi ya kuibadilisha jamii.
Wright ameyasema hayo Desemba 21, 2022 mjini Bagamoyo mkoani Pwani wakati wa kufunga mafunzo ya miezi mitatu kwa wanawake wajasiriamali kutoka Wilaya ya Bagamoyo na Mkoa wa Dar es Salam.
Mafunzo hayo ambayo yamefadhiliwa na Serikali ya Marekani kupitia programu ya Mafunzo kwa Wajasiriamali wanawake (Academy of Women entrepreneurs-AWE) ambayo inalenga kuwapa elimu na ujuzi na kuwajengea mtandao na kufungua fursa wanazohitaji ili kuwabadilisha mawazo yao na kuwa miradi halisi ya kuwaletea kipato.
“Jitihada za Wanawake huwa na matokeo makubwa zaidi kwa jamii nzima kwasababu wanawake wanapofabikiwa watawekeza mapato yao katika familia na jamii zao, mafanikio yenu kiuchumi yatasaidia vizazi vijavyo na ubunifu wenu utaleta matokeo chanya kwa jamii na uchumi wa Tanzania” alisema.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Nickson Saimon alipongeza Serikali ya Marekani kwa kupitia programu yake ya AWE kuwezesha mafunzo hayo ambayo anaamini yatabadili uendeshaji wa shughuli za wanawake hao.
Saimon amesema pamoja na Serikali kutoa mikopo lakini bado kuna kikwazo kwani asilimia kubwa ya biashara za wajasiriamali zinakufa na wengine wakikeama kurejesha fedha walizokopa.
Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Jesca Simon alipongeza uwepo wa programu hiyo ambayo iinakwenda kuwaimarisha wanawake Wajasiriamali.
Jesca aliomba programu hiyo iwafikie na wataalamu ambao wanafika vijijini kuelimisha vikundi vya makundi yanayonufaika na mikopo ya Halmashauri.
Kwa upande wake, Mratibu wa AWE Tanzania, Dkt. Victoria Kisyombe ameeleza kuwa, wahitimu wa mafunzo ya wanawake wajasiriamali wameonesha mfano wa kuigwa kwa kujituma kwao na kutambua kwamba wamepata fursa adimu na adhimu katika mapambano ya kibiashara.
Kufuatia hilo, Dkt. Kisyombe ametoa rai kwa kwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge kuendelea kuwalea, kuwaimarisha na kuwapatia wahitimu hao fursa zaidi za kifedha na nyinginezo zilizopo mkoani mwake katika kuhakikisha kwamba chachu iliyoanzishwa kwa msaada wa serikali ya Marekani iweze kuwafikia wa awake wengi Zaidi.
Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wanawake wajasiriamali, Dkt. Kisyombe amesema
“Ni heshima yetu kubwa kukishukuru Mhe. Balozi Dkt. Donald Wright kwa moyo wako uliojaa mapenzi mema ya kuwaendeleza wanawake, kwani umeendelea kulea na kuwezesha mafunzo haya kuwa na matokeo mazuri sana. Tunashukuru sana”
“Kazi hii ni sehemu muhimu ya serikali ya Marekani kuchangia juhudi kubwa inayofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kuinua maendeleo ya wanawake kiuchumi na hivyo kuwawezesha wanawake kuwa washiriki muhimu katika kujenga uchumi wa nchi yetu”
Kwa upande wake, mmoja wahitimu wa mafunzo hayo, Bi. Felista Mauya kutoka Elan Farm ameushukuru taasisi ya AWE na ubalozi wa Marekani kwa kuwajengea uwezo ambao utaenda kuboresha shughuli zao za ujasiriamali tofauti na ilivyokuwa awali.
Alisema pamoja na kuwa na fani yake ya sheria lakini alilazimika kuingia kwenye kilimo na ufugaji ambapo pia amekuwa akiwafundisha Vijana kujikwamua kiuchumi kupitia shughuli hizo.
” Tangu nimeanza ufugaji na kilimo nimetumia nafasi yangu kuanza kuwafundisha vijana kusaidia familia zao kujikwamua na umasikini, mafunzo haya niliyopata yataenda kuniimarisha zaidi katika shughuli zangu” alisema Mauya.
Mauya alisema ni wakati sasa Vijana kuangalia fursa zilizopo na kuzitumia ili waondoke kwenye utegemezi, kuondoa dhana ya kusubiri kuajiriwa ambayo itawawezesha kubadili maisha ya familia zao.
Mwisho