*************************
Na Mwandishi wetu, Mirerani
Wafanyabiashara wakubwa wa Madini ya Tanzanite wanaochimba na kununuwa madini katika Mji wa Mirerani Wilayani, Simanjiro Mkoani Manyara wamehamasishwa kuwekeza katika sekta ya elimu katika wilaya ya Simanjiro lengo likiwa kuinuwa elimu katika Wilaya hiyo yenye wakazi wengi wa jamii ya kifugaji na eneo ambalo linalowanufaisha katika biashara.
Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Dk Suleman Serera ameyasema hayo kwenye mahafali ya darasa la saba ya shule ya msingi ya Glisten inayomilikiwa na Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji madini Mkoa wa Manyara (MAREMA) Justin Nyari na kusema kuwa kufanya vizuri kwa shule hiyo ni sifa kwa Serikali ya Wilaya na Mkoa wa Manyara.
Serera amesema wakati umefika kwa wawekezaji hususani wafanyabiashara wa Tanzanite kuwekeza katika elimu kwani kunaweza saidia vijana kupata elimu bora na kuwa viongozi wa baadae na hilo limeonyeshwa mwanga na Nyari kwa kuwekeza katika elimu.
Kutokana na hali hiyo, Mkuu huyo wa Wilaya amewataka Wafanyabiashara wengine kuiga mfano wa Nyari aliyejitosa katika kuwekeza katika elimu kwani elimu ni msingi wa maisha na uwekezaji huo ni mzuri kwa jamii ya wakazi wa simanjiro yenye kwa kuwa asilimi kubwa ni jamii ya wafugaji.
Akizungumzia kufanya vizuri kwa shule hiyo kwa kuwa wa kwanza kiwilaya na Mkoa katika kufanya vyema mitihani ya darasa la saba, Mkuu wa Wilaya amewataka wazazi sasa kuacha kuwapeleka watoto nje ya nchi kusaka elimu kwani kuna baadhi ya shule kama hii ina walimu wazuri wenye kutoa elimu bora hivyo kuacha kasumba hiyo mara moja.
Serera amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dk Samia Suluhu Hassan inajali sana elimu kwa vijana wetu hivyo basi ili kumuunga mkono wakati ufiki kuacha kupeleka nje vijana kwa kuwa elimu inayotolewa hapa nchini ni bora zaidi.
Mmiliki wa Shule hiyo, Justin Nyari amemshukuru Mkuu wa Wilaya kwa kukubali kuwa mgeni rasmi na pia yeye kama mmiliki wa shule hiyo na walimu kwa ujumla hawataweza kubweteka na ufaulu huo kwani ndiyo kwanza wataongeza jitihada zaidi.
Nyari amesema sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa na Serikali katika sekta ya elimu inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan wanazizingatia na ndiyo maana kwa kiasi kikubwa wanafanya vyema katika kufaulisha wanafunzi.
Mmoja wa wazazi wa shule hiyo, Awadhi Masoud amemtaka mmiliki wa shule na walimu kuongeza jitihada zaidi za kutoa elimu bora kwa wanafunzi kwani kushika nafasi ya kwanza kiwilaya na Mkoa ni chachu ya wao kujipanga zaidi miaka yote ijayo.
Amesema mwaka jana shule ilishika nafasi ya tano katika kumi bora kimkoa na mwaka huu imeshika nafasi ya kwanza na huenda kitaifa ilifanya vema hivyo moto usiwe moto wa mabua uwe moto wa gesi wa kila miaka yote ijayo na siyo vinginevyo.