Na. WFA
Katibu Wizara ya Afya, Prof. Abel Makubi amesema kuwa Serikali katika kupambana na ugonjwa wa Saratani wamejipanga kushirikiana na sekta zingine hasa Wizara ya Elimu na Fedha nchini ili kuwekeza na kupanua huduma za Saratani nchini.
Prof. Makubi ametoa kauli hiyo leo Jijini Dodoma katika kikao kazi kilichoshirikisha sekta hizo ili kupitia andiko la ufadhili wa uwekezaji na upanuzi wa Huduma za Saratani nchini. Wizara ya Afya kwa sasa ipo katika mkakati ya kushusha huduma za Saratani katika ngazi ya Kanda na mikoa pia kuvutia utalii tiba kutoka nchi za jirani.
Prof. Makubi ametoa wito kwa sekta zote tatu kuwa na ushirikiano wa kisekta katika kuratibu utafutaji wa ufadhili wa fedha za kutekeleza mradi wa kusogeza huduma za Saratani katika hospital za rufaa za kanda na mikoa.
Andiko la upanuzi wa huduma za saratani nchini linagharimu shilingi za Kitanzania billioni 240 kwa ajili ya miundombinu, vifaa, watalamu, mafunzo na kinga na inategemewa Serikali itasaidiana na wadau mbalimbali na sekta binafisi katika kufanikisha uwekezaji huo.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Katibu Mkuu wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Mukajungu Kamuzora amesema wako tayari kushirikiana kutafuta wafadhili ili kufanikisha upatikanaji wa huduma hizo karibu na wananchi.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Dkt. Julius Mwaisalage ameishukuru Serikali na kusema kuwa iwapo andiko ilo litapita na kutekelezwa kikamilifu itasaidia kupunguza msongamano wa wagonjwa wa saratani katika Hospitali ya Ocean Road kwani huduma za kibingwa zitakuwa zimesogezwa karibu na wananchi.