Na Mwandishi wetu, Mirerani
WANACHAMA wa kikundi cha Nyanza Group cha Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wametunisha mfuko wao kwa kukusanya shilingi milioni 4.8 kwenye uzinduzi wa fulana na kalenda zao za mwaka 2023.
Mwenyekiti wa Nyanza Group, Malimi Kija akiongoza shughuli ya uzinduzi huo amesema wanachama hao wamejitoa na kuchangia kiasi hicho cha fedha hizo.
Kija amesema kila mwanachama amechangia shilingi elfu 30 kwa kununua fulana na kalenda ila wenye kipato kikubwa wamenunua kwa shilingi laki 5, laki 2, laki moja na elfu 50.
“Niwapongeze na kuwashukuru wanachama wote ambao kwa namna moja au nyingine mmeshiriki kutunisha mfuko wetu wa Nyanza Group,” amesema Kija.
Amesema katika kutunisha mfuko wao wamepata fedha taslimu shilingi milioni 4 laki moja na elfu 70 na ahadi shilingi 725,000 hivyo kufikisha shilingi 4,895,000.
Amesema kadiri miaka inavyozidi kwenda ndivyo umoja wao unavyozidi kupiga hatua hivyo Nyanza Group ni kikundi kikubwa cha kuigwa mfano.
Afisa maendeleo ya jamii wa Mji mdogo wa Mirerani Isack Mgaya amesema kikundi hicho kimekaa muda mrefu kwa zaidi ya miaka 20 hivyo wanapaswa kuupongezwa.
Mgaya amesema baadhi ya vikundi vingine vimekufa kutokana na uongozi mbovu ila Nyanza Group wamefanikiwa kukaa muda mrefu bila migogoro.
Hata hivyo, amewataka wanachama hao kujihusisha na mikopo mbalimbali ikiwemo inayotolewa na halmashauri ambayo itawawezesha na kunufaika kiuchumi.
“Kwenye halmashauri kuna makundi ya wanawake, vijana na walemavu wanapatiwa mikopo hivyo undeni vitengo vya namna hiyo ili kujinufaisha kiuchumi,” amesema Mgaya.