Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha
HALMASHAURI ya Mji Kibaha inatarajia kufungua kituo jumuishi cha huduma za pamoja (One Stop Centre) , ifikapo Januari 2023 ili kuwarahisishia wajasiriamali kurasimisha biashara zao.
Akizungumza na waandishi wa habari Kaimu Mkuu wa Idara ya Viwanda Biashara na Uwekezaji wa Halmashauri ya Mji Kibaha ,Adolf Msangi wakati wa mafunzo ya namna ya uboreshaji wa biashara ili ziweze kurasimishwa na kukidhi vigezo vya ushindani wa biashara kwenye soko.
Msangi alifafanua , kituo hicho cha huduma za pamoja kitakuwa na Taasisi wezeshi zote ambazo zinahusika katika kurasimisha biashara ili kuwaondolea usumbufu wafanyabiashara kusajili biashara zao.
“Kituo hichi kwa sasa kiko hatua za mwisho ambapo ni hatua ya manunuzi na Januari mwakani kituo kitaanza kazi na kitawarahisishia wajasiriamali badala ya kwenda ofisi sehemu tofauti watakuwa wanakwenda sehemu moja na kumaliza usajili sehemu moja,”alisema Msangi.
Alieleza, kituo hicho kitakuwa na Taasisi zikiwemo Tra, mabenki, Osha, bima, Latra na Taasisi zinazohusika na masuala ya biashara na usimamizi zote zikiwa kwenye jengo moja.
Kwa upande wake ofisa utawala kutoka MKURABITA Joseph Temanya alisema kuwa lengo la kuwarasimisha wafanyabiashara wadogo ni kuweza kufikia fursa za mikopo, ujuzi wa uendeshaji biashara ,masoko na uboreshaji bidhaa na biashara zao.
Naye Mwenyekiti wa Wamachinga Mkoa wa Pwani Philemon Maliga alieleza, kuanzishwa kwa kituo hicho itawarahisishia kupata usajili kwa urahisi kwani zamani walikuwa wanapata usumbufu kuzunguka sehemu mbalimbali kwa ajili ya urasimishaji biashara.