Baadhi ya akina mama wa kijiji cha Ilela Halmashauri ya wilaya Ludewa mkoani Njombe ambao hawakufahamika majina yao mara moja,wakichota maji katika moja ya vituo vilivyojengwa kwenye mradi wa maji katika kijiji hicho.
Mkazi wa kijiji cha Ilela Halmashauri ya wilaya Ludewa mkoani Njombe Daud Malongo kushoto,akimueleza Meneja wa Ruwasa wilaya ya Ludewa Mhandisi Mlenge Nassibu kuhusu uwezo mdogo wa tenki la kuhifadhi maji lililojengwa katika kijiji hicho.
Tenki lenye uwezo wa kuhifadhi maji lita 50,000 ambalo linatosheleza kwa mahitaji ya wananchi wa kijiji cha Ilele wilayani Ludewa.
***********************
Na Muhidin Amri, Ludewa
WAKAZI wa kijiji cha Ilela wilaya ya Ludewa mkoani Njombe waliokuwa wanakabiliwa na kero ya maji safi na salama,wameondokana na adha hiyo baada ya wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)kukamilisha ujenzi wa mradi wa maji.
Mradi huo ambao umekamilika kwa asilimia 100 unakwenda kuwanufaisha zaidi ya wakazi 980 wa kijiji hicho ambao hawajahi kupata maji ya bomba tangu Uhuru,badala yake walitumia maji ya ziwa nyasa yanayopatikana umbali wa km 1.
Meneja wa Ruwasa wilaya ya Ludewa Mhandisi Mlenge Nassibu alisema, chanzo cha mradi huo ni kisima kirefu na umejengwa kwa mfumo wa force akaunti kwa gharama ya Sh.milioni 180.
AidhaNassibu alisema, mbali na mradi huo Ruwasa imetekeleza mradi mwingine katika kijiji cha Kipingu na Ngelenge miradi ambayo inaendeshwa kwa umeme wa jua(solar),hata hivyo wako katika hatua ya mwisho ya kubadilisha matumizi ya solar ili uweze kutumia umeme wa Tanesco.
Nassibu,ameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji katika maeneo mbalimbali ya wilaya ya Ludewa na kuhaidi kusimamia vizuri matumizi ya fedha na ujenzi wa miradi ya maji inayokwenda kumaliza kabisa changamoto ya maji safi na salama kwa wananchi.
Diwani wa kata ya Ruhuhu Athanas Haule alisema,mradi huo wa maji ni ukombozi mkubwa kwa wananchi wa kijiji hicho hasa wakati wa kiangazi kwa kuwa wakati wa masika wananchi wanatumia maji yanayotiririka kutoka milimani.
Alisema,kabla ya kujengwa kwa mradi huo wananchi wa Ilela walilazimika kutumia maji ya visima vifupi na ziwa nyasa ambayo sio safi na salama kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi na shughuli mbalimbali za kibinadamu.
Ameishukuru serikali kupitia wakala wa maji safi na usafi wa mazingira(Ruwasa), kutoa fedha ambazo zimefanikisha kujengwa kwa mradi huo na kumaliza mateso ya muda mrefu kwa wananchi wa kijiji hicho kutembea umbali mrefu kwenda kutafuta maji.
Kwa upande wake katibu wa chombo cha watoa huduma ya maji ngazi ya jamii(CBWSO) William Kunyanja alisema, tangu chombo kilipoanzishwa kumekuwa na manufaa mengi kwa wananchi kupata huduma ya maji safi na salama ikilinganisha na hapo awali.
Alisema,tangu chombo hicho kilipoanzishwa mwezi Julai mwaka huu jumla ya wananchi 15 wameingiza maji majumbani na wanaendelea kupokea maombi kutoka kwa wananchi wengine walioonesha nia ya kuingiza maji majumbani badala ya kutumia vituo vya umma.
Alitaja gharama ya kulipia huduma ya maji kwa kila kaya ni Sh.1000 kwa mwezi na katika kijiji hicho kinakadiriwa kuwa na kaya kati ya 2,800 hadi 3,000 ambazo zinapata maji safi na salama katika maeneo yao.
Mkazi wa kijiji cha Ilela Mariam Mbeya,ameipongeza Ruwasa kukamilisha mradi huo ambao umewaondolea kero ya kuamka usiku wa manane kwenda kutafuta maji kwenye visima vya asili ambavyo havikutosheleza mahitaji yao.
Hata hivyo,ameiomba Ruwasa kuongeza idadi ya vituo vya kuchotea maji ili kusogeza huduma hiyo karibu na makazi yao kwani vilivyopo havitoshi kulingana na idadi ya watu waliopo katika kijiji hicho.
MWISHO.