Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel amewaomba wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini kuendelea kushirikiana na Mhimili huo katika kutoa elimu juu ya vitendo vya ukatili wa kijinsia na mauaji ili kuweza kupunguza matukio hayo.
Kauli hiyo imetolewa na Mtendaji huyo, mwisho mwa wiki iliyopita katika mkutano wake na wahariri hao uliofanyika kwenye ukumbi wa mkutano wa Kituo wa Jumuishi cha Utoaji Haki cha Masuala ya Familia, kilichopo Temeke Jijini Dar es Salaam baada ya baadhi ya wahariri kuuliza Mahakama inachukua hatua gani za kupunguza vitendo hivyo.
“Mahakama inaendelea kutoa elimu kwa wadau kupitia vipindi mbalimbali mfano cha mubashara cha kinachojulikana kwa jina la ‘Sema na Mahakama ya Tanzania’ kinachorushwa na Televisheni ya Taifa (TBC1) kila alhamisi saa 12:00 jioni hadi saa 1:00 usiku na Kituo cha Televisheni ya (ITV) kuanzia saa 12:00 jioni hadi saa 1:30 usiku.
‘‘Lakini elimu hiyo haipaswi kutolewa na Mahakama pekee inatakiwa ushirikiano wa pamoja kutoka kwa viongozi wa dini, vya habari na kadhalika, hivyo tunaomba na nyie muendelee kusaidia kutoa elimu hiyo,” alisema Mtendaji Mkuu huyo.
Katika hatua nyingine akijibu hoja kuhusu mashauri ya ardhi yanayoendeshwa na Wazee wa Baraza la Ardhi na gharama zake, Mkuu wa Kitengo cha Maboresho ya Mahakama ya Tanzania, Dkt. Angelo Rumisha amesema baraza hilo haliko chini ya Mahakama.
Aliongeza kuwa baraza hilo liko chini ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mwenyekiti wa barza hilo anateuliwa na Waziri husika.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Bw. Deodatus Balile amesema milango iko wazi kwa Mahakama kuendelea kushirikiana na TEF kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu wananchi.