**********************
Na Muhidin Amri,
Ludewa
WATUMISHI wa zahanati ya kijiji cha Nkomang’ombe Halmashauri ya wilaya Ludewa mkoani Njombe,wameondokana na kero ya kutembea umbali wa km 10 kila siku kwenda kuchota maji mto Mchuchuma kwa ajili ya matumizi mbalimbali ikiwamo usafi na matumizi ya wagonjwa wanaofika kupata huduma ya matibabu.
Sasa kero hiyo imekwisha baada ya wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa),kujenga mradi mkubwa wa maji katika kijiji cha hicho huku zahanati hiyo ikijengewa kituo kimoja cha kuchotea maji ambacho kimekuwa mkombozi kwa watumishi.
Mganga Mfawidhi wa zahanati hiyo Sifael Mpolo alisema,kabla ya mradi huo walilazimika kwanza kwenda mtoni kutafuta maji kabla ya kuanza kuhudumia wagonjwa, hivyo kuathiri sana kazi utoaji huduma za matibabu kwa wananchi.
Dkt Mpolo alisema,kufikishwa kwa huduma ya maji safi na salama katika kijiji hicho imesaidia watumishi kutekeleza majukumu yao kwa wakati kwa kuwa hawapaswi kwenda mtoni kuchota maji,badala yake wanatumia maji kutoka kwenye kituo kilichojengwa na Ruwasa.
Aidha alisema,mradi wa maji ya bomba umesaidia sana kupungua kwa baadhi ya magonjwa ikiwamo matumbo,kuharisha na kichocho yaliyo sababishwa na matumizi ya maji yasio safi na salama kwa wananchi wa kijiji hicho.
Dkt Mpolo,ameishukuru serikali kupitia Ruwasa kujenga mradi huo ambao umewezesha watumishi kupata muda wa kutosha,kufanya kazi kwa kujituma na weledi mkubwa ambapo amehaidi kutumia fursa hiyo kutoa huduma bora kwa wananchi.
Meneja wa Ruwasa wilaya ya Ludewa Mhandisi Mlenge Nassibu alisema,mradi wa maji Nkomang’ombe umetekelezwa kwa gharama ya Sh.milioni 750 na unahudumia wananchi 3,500 wa vijiji viwili vya Kimelembe na Nkomang’ombe.
Alisema,katika mradi huo wamejenga matenki mawili mapya na kukarabati tenki moja la zamani sambamba na ujenzi wa vituo 14 vya kuchotea maji katika maeneo mbalimbali ya vijiji hivyo na wananchi wameanza kutumia maji hayo kwa ajili ya shughuli mbalimbali.
Mtendaji wa kata ya Nkomang’ombe Tumaini Ng’ande alisema,kupatikana kwa mradi huo kumemaliza migogoro mingi na ya mara kwa mara ya ndoa iliyosababishwa na wanawake kuchelewa kurudi nyumbani kutoka kutafuta maji kwa ajili ya matumizi ya familia zao.
Aidha alieleza kuwa,mradi wa maji ya bomba umewasaidia wananchi wa kata hiyo kupata muda mwingi wa kufanya kazi za maendeleo ikiwamo ujenzi wa nyumba bora na kushiriki shughuli mbalimbali za kijamii.
Baadhi ya wanawake wa kijiji hicho,wameishukuru Serikali kupitia Ruwasa wilaya na mkoa wa Njombe kumaliza kero ya muda mrefu na kutumia muda mwingi kwenda kutafuta maji kwenye vyanzo vya asili na kumaliza vitendo vya ngono na migogoro kwenye ndoa zao.
Ostazia Mgaya alisema,siku za nyuma walilazimika kuamka usiku kati ya saa 9 na saa 10 alfajiri kwenda kutafuta maji katika mto Mchuchuma unaopatikana umbali wa km 10 na kurudi saa 4 au 5 asubuhi.
Alisema,kero hiyo ili sababisha kushindwa kushiriki kikamilifu kwenye shughuli mbalimbali za maendeleo na wakati mwingine kukosa nafasi ya kuhudumia familia zao majumbani.
Ester Haule, ameipongeza Ruwasa kukamilisha mradi huo ambao umeokoa ndoa za wanawake wengi wa kijiji hicho,hata hivyo ameiomba serikali kuendelea kuboresha baadhi ya huduma muhimu za kijamii ili kutoa fursa kwa wananchi kushiriki vyema shughuli mbalimbali za kiuchumi.