******************
Na Zillipa Joseph, Katavi
Halmashauri ya Nsimbo ilyopo katika wilaya ya Mpanda mkoani Katavi imeanza mpango wa upandaji wa miti ya matunda katika taasisi mbalimbali za elimu zikiwemo shule za sekondari na vyuo kwa lengo la kupiga vita udumavu.
Akizungumzia mpango huo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Nsimbo Mohamed Ramadhan alisema lengo ni kuwaandaa vijana hasa wa kike ambao ndio wazazi wa baadae kuwa na miili yenye afya njema hata watakapokuja kupata watoto waelewe umuhimu wa kula vyakula vyenye mchanganyiko wa makundi tofauti.
“Ukiacha zoezi hili la kupanda miti hii ambayo tumetaka kila mwanafunzi anayepanda mti apewe jukumu la kuulea mti huo mpaka ukue pia tutaanzisha bustani za mbogamboga ambazo zitasaidia kurahisisha upatikanaji wa mahitaji ya mboga shuleni tofauti na ilivyozoeleka sasa kwamba wanafunzi ni wa kulishwa ugali na maharage pekee” alisema Mohamed.
Bi. Mwanaidi Selemani ni Afisa Lishe katika halmashauri ya Nsimbo amesema tatizo la udumavu kwa watoto katika halmashauri hiyo linasababishwa na wazazi kutokuwa na uelewa wa namna ya kulisha watoto hata na wao kutambua umuhimu wa kula vyakula tofauti licha ya kuwa vyakula vingi vinapatikana katika maeneo yao.
Aliongeza kuwa jamii imekuwa na mazoea ya kutokula mboga za majani kwa kudhani ni mboga kwa ajili ya watu wenye hali duni, jambo ambalo si sawa hali inayopelekea kuwa na watoto wengi wenye udumavu.
Bi. Mwanaidi alisema zoezi hilo litasaidia wanafunzi kuwa na uelewa wa kutosha wa umuhimu wa lishe bora hali itakayosaidia wao kuja kuwa wazazi bora na matumaini ni kwamba tatizo la utapiamlo litapungua mkoani Katavi.
Dokta Venanda Msati ni Mganga Mfawidhi katika kituo cha Afya cha Katumba alisema zaidi ya watoto 10 hadi 15 wenye umri wa chini ya miaka mitano wanalazwa kwa mwezi katika kituo hicho kwa sababu ya utapiamlo mkali huku watoto wengine kati ya 30 hadi 40 wanatibiwa na kuruhusiwa kutokana na tatizo hilo la utapiamlo.
Dk. Msati alisema kwa watoto wenye utapiamlo wa kawaida wanapatiwa chakula dawa na kuwaelimisha wazazi namna ya kuwaandalia chakula watoto wao ili waweze kuwa na hali nzuri.
Aidha kwa watoto wenye utapiamlo mkali wanalazwa na kupatiwa chakula dawa mpaka watakapopata nafuu na baadaye wanaruhusiwa kutoka hospitali.
Dk. Msati amesema chanzo kikuu cha utapiamlo ni wazazi kutingwa na kazi nyingi na hivyo kushindwa kuwa na uangalizi mzuri wa watoto wao.
‘Wazazi wanajali sana kwenda kufanya kazi za vibarua na kuwaacha watoto wadogo chini ya uangalizi wa watoto wenzao hali inayopelekea kushinda wakila viporo’ alisema.
Aliongeza kuwa mtoto akiugua kwa muda mrefu hatimaye anadumaa na hali hiyo inapelekea mtoto kuwa mzito kwa kila jambo hasa katika ukuaji wake.
Wakizungumzia zoezi la upandaji miti katika shule ya sekondari ya wasichana ya Nsimbo wanafunzi wa shule hiyo akiwemo Betilda Magego na Hilda Mwamsumba walisema wanafurahia zoezi hilo kwani sasa wana uhakika wa kuanza kupata mlo kamili baada ya miezi michache.
Wanafunzi hao wametaja miche ya miti ya matunda waliyopanda kuwa ni pamoja na mipapai, mipera, pasheni na miparachichi.
Bwana Oswald Kapama ni Afisa misitu wa Halmashauri hiyo ambaye alisema halmashauri itapanda zaidi ya miti 1500 ya matunda katika taasisi mbalilmbali katika msimu huu wa mvua.
Naye mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Mpanda katika zoezi hilo; Afisa Tarafa wa Misunkumilo Bi. Leah Gawaza amesema zoezi hilo linafanyika katika kumuunga mkono mheshimwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika jitihada za kuinua hali ya lishe hapa nchini.