Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Jenifa Omolo akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kwenye mahafali ya 36 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini Duru ya pili yaliyofanyika kwenye kituo cha mafunzo cha kanda ya ziwa Jijini Mwanza
Mwenyekiti wa Baraza la uongozi wa Chuo Profesa Martha Qorro akizungumza kwenye mahafali ya 36 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini
Baadhi ya wahitimu kutoka Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini wakiwa kwenye mahafali
Picha ya pamoja
……………………………….
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Wizara ya Fedha na Mipango imezitaka taasisi za elimu ya juu na kati kuwa na moduli ya masuala ya ujasiriamali katika kozi zao ili kuweza kuwaandaa vijana kuwa wataalamu katika nyanja mbalimbali.
Rai hiyo ilitolewa jana Disemba 16,2022 na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Jenifa Omolo, kwenye mahafali ya 36 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini Duru ya pili katika kituo cha mafunzo cha Kanda ya ziwa Jijini Mwanza.
Omolo amesema kozi zinazotolewa na Chuo cha Mipango zina moduli ya masuala ya ujasiriamali hivyo anaamini wahitimu wametambua kuwa msingi mkubwa wa ujasiriamali ni wazo na si fedha.
Amewaasa wahitimu kuyafanyia upembuzi yakinifu mawazo yao ya biashara waliyonayo kwa kuyaandalia mpango wa biashara na kuyatekeleza kwa ufanisi.
” Nawaomba muwe na moyo wa kuthubutu kuyafanyia kazi maono yenu na katu msiogopeshwe na watu wachache ambao walikuwa na mawazo kama yenu lakini wakashindwa kuyaendeleze”, amesema Omolo
Aidha, ameeleza kuwa Serikali iko tayari kusaidia vijana wenye mawazo chanya ya kibishara kutimiza malengo yao, jambo la muhimu ni kujiunga kwenye vikundi vyenye lengo la aina moja ili iwe rahisi kukabiliana na changamoto ya mtaji mdogo kwa kushirikiana na wengine kiliko mtu akiwa peke yake.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo hicho Prof Hozen Mayaya, amesema katika kuunga mkono juhudi za Serikali kwenye masuala ya elimu wataendelea kuwaandaa wataalamu wenye weledi wa kutosha katika fani za mipango ya maendeleo sanjari na kutoa huduma iliyo bora kwa wakati na inayokidhi matakwa ya wadau wao.
Mwenyekiti wa Baraza la uongozi wa Chuo hicho Prof, Martha Qorro ametoa wito kwa jamii kuwapokea wanafunzi waliohitimu ili waweze kufanya nao kazi kwa ukaribu hususani katika uandikaji wa miradi mbalimbali.
Nao wahitimu wametoa shukurani kwa uongozi wa Chuo kwanamna ambavyo wamewaandaa vizuri kwenda kupambana na soko la ajira.