Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na watumishi wa umma katika Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi katika halmashauri hiyo.
Watumishi wa Umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi mkoani Singida wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi hao.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Peter Serukamba akitoa salamu za mkoa wake kabla ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kuzungumza na watumishi wa umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri huyo iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi katika halmashauri hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Mhe. Jerry Muro akieleza hali ya Utumishi wa Umma katika wilaya yake kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya waziri huyo iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi katika Wilaya ya Ikungi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akisalimiana na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida, Bi. Martha Mlata katika Ofisi za CCM mkoani humo, mara baada ya Waziri huyo kuwasili mkoani Singida kwa ajili ya ziara ya kikazi.
………………………………….
Na. James K. Mwanamyoto-Ikungi
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amekemea tabia ya baadhi ya waajiri Serikalini kutoa kipaumbele cha kulipa madeni yasiyo ya mishahara kwa Wakuu wa Idara pekee na kuyaacha ya watumishi walio wengi, kitendo ambacho kinashusha ari na morali ya utendaji kazi wa watumishi wa umma nchini.
Mhe. Jenista amekemea tabia hiyo wakati wa kikao kazi chake na watumishi wa umma katika Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi mkoani Singida kilicholenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi katika halmashauri hiyo.
Mhe. Jenista amesema, kama mwajiri amekusanya mapato na ana lengo la kulipa madeni yasiyotokana na mishahara, anapaswa kutenda haki kwa kuweka usawa katika kulipa madeni ya watumishi na Wakuu wa Idara badala ya kutoa kipaumbele kwa Wakuu wa Idara pekee.
“Si haki kwa Wakuu wa Idara kutengenezewa mkakati wa kulipwa peke yao na watumishi wengine kutolipwa na ikizingatiwa kuwa wanatoa mchango mkubwa katika kuwahudumia wananchi,” Mhe. Jenista amefafanua.
Mhe. Jenista ameongeza kuwa, kitendo cha waajiri kulipa madeni ya Wakuu wa Idara pekee, amekuwa akikikemea mara kwa mara wakati wa vikao kazi vyake na waajiri kwani kinaathiri saikolojia ya utendaji kazi wa watumishi wa umma na kukwamisha lengo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan la kutoa huduma bora kwa wananchi.
“Waajiri msijali sana maslahi ya Wakuu wa Idara na kusahau kuzingatia maslahi, haki na stahiki za watumishi wa umma ambao ni wengi kuliko Wakuu wa Idara hivyo, mnapaswa kuzingatia agizo hili,” Mhe. Jenista amesisitiza.
Akizungumzia madeni ya malimbikizo ya mishahara, Mhe. Jenista amesema madeni hayo yamezingatiwa na Serikali kwani Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alielekeza itengwe fedha jambo ambalo lilitekelezwa na katika mwaka wa fedha ujao itatengwa pia ili kuendelea kuwalipa watumishi wanaostahili, na kuongeza kuwa ofisi yake imejipanga kuhakiki madai yote yatakayowasilishwa ili yalipwe kwa wakati.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Peter Serukamba ameunga mkono maelekezo ya Mhe. Jenista Mhagama, na kuwashauri waajiri kuanza kulipa madeni ya watumishi wa umma walio wengi kwani wakianza kuwalipa Wakuu wa Idara ambao kila mmoja anadai fedha nyingi, sehemu kubwa ya makusanyo itaishia kulipa madeni ya Wakuu wa Idara pekee.
“Watumishi walio wengi wanadai kiasi kidogo cha fedha ukilinganisha na Wakuu wa Idara, hivyo, wakilipwa hao kwanza, watabakia Wakuu wa Idara ambao wanadai fedha nyingi, na hata kama wakuu hao wakilipwa mmoja mmoja kiasi chote cha fedha wanachodai wataona thamani ya fedha waliyokuwa wakiidai,” Mhe. Serukamba amefafanua.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Mhe. Jerry Muro amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwaletea maendeleo wananchi wa Ikungi, kitendo ambacho kimejenga morali ya utendaji kazi wa watumishi wa umma walio katika wilaya yake ambao kwa kiasi kikubwa wamechangia kukusanya mapato yatakayoisaidia Serikali kuendelea kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amehitimisha ziara yake ya kikazi mkoani Singida, ambayo ililenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma, kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma, kukagua utekelezaji wa majukumu ya Chuo cha Utumishi wa Umma pamoja na utekelezaji wa Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini mkoani humo.