Mkaguzi Mkuu wa ndani wa serikali ,Athumani Selemani Mbuttuka akizungumza katika mahafali hayo jijini Arusha leo.
Baadhi ya wahitimu katika chuo cha uhasibu Arusha wakiwa katika mahafali yao jijini Arusha leo.
********************
Julieth Laizer,Arusha.
Arusha.Mkaguzi Mkuu wa ndani wa serikali,Athumani Selemani Mbuttuka ametoa wito kwa vyuo nchini kufanya mabadiliko ya mitaala yao ili kuwezesha ufundishaji kwa vitendo ili kuendana na mahitaji ya soko .
Ameyasema hayo leo jijini Arusha wakati akimwakilisha Waziri wa fedha,Dk Mwigulu Nchemba katika mahafali ya 24 ya wanafunzi wa chuo cha uhasibu Arusha (IAA) ambapo jumla ya wanafunzi 3,529 wamehitimu kozi mbalimbali.
Amesema kuwa,mafunzo kwa vitendo bado hayapewa umuhimu katika vyuo mbalimbali ,hivyo ni wajibu wao kuhakikisha wanafanya mabadiliko ili kuondokana na changamoto ya ajira .
“Tunaomba pia vyuo vyetu wahakikishe wanajikita kwenye maswala ya tabia ya nchi katika kuhakikisha kunakuwepo na mitaala vyuoni ili wanafunzi waweze kufahamu wakiwa vyuoni, huku akivitaka vyuo kujikita katika kufanya taifiti kwenye rasilimali na uimarishaji wa fedha”amesema .
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa chuo cha uhasibu Arusha , Dk .Cairo Mwaitete
amesema kuwa,chuo hicho kimepiga hatua kubwa kwa kuwa na wanafunzi wengi kutoka wanafunzi 3,000 mwaka 2017/18 hadi wanafunzi 13,000 kwa mwaka huu wa fedha ,na kimekuwa kikifanya tafiti mbalimbali ambazo zina lengo la kutoa elimu bora itakayosaidia kutatua changamoto katika jamii.
Mwaitete amesema kuwa,chuo hicho kimejiwekea mikakati ya kuongeza mitaala mingine katika ngazi ya astashahada na shahada kwa lengo la kuwafikia wengi zaidi na kwenda kutatua changamoto katika jamii.
“Tumeona kuna haja ya kujipanua zaidi na hivyo tunaangalia namna ya kushirikiana na jeshi la polisi katika kutoa elimu juu ya matumizi ya kompyuta na vifaa ili kuweza kuwaandaa walinzi wa mitandaoni watakaolinda fedha zetu kwenye mabenki.”amesema Mwaitete.
Ameongeza kuwa ,wanataka kuhakikisha wanaendelea kusaidiana na serikali katika kuandaa mafunzo ya usalama na taarifa na kujiepusha na makosa mbalimbali yanayotokea mitandaoni.
Amefafanua kuwa, chuo hicho kimekuwa kikiunga mkono sera ya serikali ya kupeleka elimu katika maeneo ya pembezoni huku wakihahakisha wanaboresha mitaala ili iweze kuendana na wakati na kuwezesha wanafunzi
Aidha amewataka wahitimu hao kuweza kujiajiri wao wenyewe huku wakizitafuta fursa mbalimbali ambazo zipo katika nchi yetu ambazo zikitumiwa vizuri zitaweza zitaweza kutatua changamoto ya ajira.
Naye Mwenyekiti wa bodi ya chuo hicho,Dk Mwamini Tulli amesema
kuwa,katika mahafali ya mwaka 2021 walikuwa jumla ya wahitimu 2,481 ambao walitunukiwa vyeti katika ngazi nne tofauti ambazo ni shahada za uzamili,shahada,stashahada na astashahada ambapo aliwataka wahitimu hao kutumia elimu yao kupambana na maisha na wasitegemee ajira bali wajiamini kuwa wanaweza ili wasiendelee kutembea na vyeti.
Mkuu wa wilaya ya Ngorongoro ambaye ni mmoja wa wahitimu, Raymond Mangwala amesema kuwa,ameweza kupata uelewa mkubwa juu ya matumizi ya Tehama kwa viongozi hususani katika usimamizi wa miradi ya maendeleo,utatuzi wa migogoro,uandaaji wa biashara ,ambapo itawezesha miradi hiyo kufanyika kwa weledi na uaminifu mkubwa .