Mkurugenzi mkuu wa hospitali ya St.Joseph ,Dk Thobias Mkina akizungumzia huduma hiyo inayotolewa na madaktari bingwa kutoka hospitali ya Apollo nchini India .
Meneja masoko wa hospitali ya Apollo kutoka nchini India,Varun Sukhija akizungumzia kuhusiana na zoezi hilo linalofanyika jijini Arusha
………………………………
Julieth Laizer ,Arusha.
WANANCHI mkoani Arusha wametakiwa kuchangamkia huduma za kibingwa zinazotolewa na madaktari bingwa wa magonjwa yasiyoambukiza kutoka ndani na nje ya nchi kwa kupima afya zao na kupata tiba ikiwemo magonjwa ya saratani.
Hayo yamesemwa jijini Arusha na Mganga mkuu wa mkoa wa Arusha ,Dk Silvia Mamkwe wakati alipohudhuria zoezi la upimaji wa magonjwa yasiyoambukiza huduma inayotolewa na madaktari bingwa kutoka hospitali ya kimataifa ya Apollo iliyopo nchini India kwa kushirikiana na hospitali ya Saint Joseph iliyopo jijini Arusha.
Dk Mamkwe amesema kuwa, kumekuwepo na ushirikiano mzuri kati ya madaktari bingwa kutoka nje ya nchi wanaokuja nchini kutoa huduma za matibabu kwa lengo la kuwapunguzia gharama wananchi kufuata matibabu nje ya nchi ,hivyo amewataka kuwa mstari wa mbele kuchangamkia fursa hiyo na kuweza kutibiwa.
“Hapo awali tulikuwa tukikakabiliwa na changamoto ya vifaa vya uchunguzi “city scan ” katika hospitali nyingi za rufaa hali iliyokuwa ikiwalazimu wananchi wengi kufuata huduma hiyo nje ya nchi ila kwa sasa hivi vifaa hivyo vipo vya kutosha ,hugo nawaomba wananchi wajitokeze kwa wingi kupata huduma.”amesema Dk Mamkwe.
Aidha amesema kuwa, takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 30 ya wananchi mkoani Arusha wanasumbuliwa na matatizo ya magonjwa yasiyoambukiza ,hivyo elimu zaidi inahitajika kutolewa kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kupima afya zao na kuweza kupatiwa matibabu ya haraka.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali ya Saint Dk Joseph Thobias Mkina amesema kuwa,idadi ya magonjwa yasiyoambukiza yamezidi kuongezeka siku hadi siku hivyo uwepo wa madaktari bingwa kutoka nchini India kunasaidia sana wananchi kuweza kupata huduma hiyo kwa haraka na kuokoa gharama ya kufuata huduma hiyo nje ya nchi.
Dk Mkina amesema kuwa, wamekuwa na ushirikiano wa karibu na madaktari bingwa kutoka hospitali ya Apollo ambapo wameweka kambi siku mbili kwa ajili ya kutoa huduma ya magonjwa mbalimbali yasiyoambukiza yakiwemo magonjwa ya saratani ya kizazi, matiti,koo,utumbo,Kansa ya damu, ngozi,ini,kibofu cha mkojo na tezi dume na magonjwa yote ya Figo.
“ujio wa madaktari hawa bingwa kutoka nchini India kunatoa fursa pia kwa madaktari wetu kuweza kujifunza zaidi kupitia wao na madaktari wetu watatoka hapa na kwenda nchini India kwa lengo la kujifunza zaidi kutoka kwao na kambi hizi zitakuwa zikifanyika kila baada ya miezi mitatu ambapo kwa awamu hii ya kwanza tunatarajia kuwafikia zaidi ya wananchi 3,000 “amesema Dk Mkina.
Kwa upande wake ,Afisa masoko kutoka hospitali ya Apollo nchini India ,Vuran Sukhija amesema kuwa,matarajio yao ni kuona wananchi wa Arusha wanahudumiwa na kupatiwa huduma nzuri za matibabu kutoka kwa madaktari bingwa wawili kutoka hospitali hiyo ya Apollo.
Nao Baadhi ya wagonjwa walionufaika na huduma hiyo ,Mery Kasian kutoka jijini Dar es Salaam na Irene Matemu wameshukuru kwa ujio huo huku wakiomba serikali kuwepo kwa kambi za mara kwa mara kutoka kwa madaktari bingwa pamoja na kuomba huduma hiyo iwe endelevu hapa nchini hususani mkoa wa Arusha kwani wananchi wenye uhitaji ni wengi.