WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Prof.Joyce Ndalichako ,akizungumza wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Chama Cha Walimu (CWT) kwa niaba ya Makamu wa Rais, Dk.Philip Mpango ulioanza leo Desemba 15,2022 jijini Dodoma.
KAIMU Rais wa CWT, Dinnah Mathamani,akizungumza wakati wa Mkutano Mkuu wa Chama Cha Walimu (CWT) ulioanza leo Desemba 15,2022 jijini Dodoma.
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi(CCM), Bara, Christine Mndeme,akizungumza wakati wa Mkutano Mkuu wa Chama Cha Walimu (CWT) ulioanza leo Desemba 15,2022 jijini Dodoma.
SEHEMU ya Walimu wakifatilia hotuba ya Makamu wa Rais iliyosomwa kwa niaba na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Prof.Joyce Ndalichako (hayupo pichani)wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Chama Cha Walimu (CWT) ulioanza leo Desemba 15,2022 jijini Dodoma.
…………………………
Na Alex Sonna-DODOMA
MAKAMU wa Rais Dk.Philip Mpango amekemea vikali udanyanyifu wa mitihani unaofanywa na baadhi ya watumishi wa Serikali wasio waaminifu na kuwataka Wakuu wa shule kutojiingiza katika udanganyifu huo.
Onyo hilo limetolewa leo Desemba 15,2022 jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Prof.Joyce Ndalichako wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Chama Cha Walimu (CWT) kwa niaba ya Makamu wa Rais, Dk.Philip Mpango.
Prof.Ndalichako,amesema kuna walimu wachache wamekuwa na tabia isiyofaa ya kushiriki katika kuvujisha na kusambaza mitihani kwa wanafunzi kwa maslahi yao binafsi au kupandisha hadhi ya shule ionekane ina ufaulu mzuri.
“Niwaonye walimu wa namna hii kuacha tabia hii na badala yake wafanyekazi kwa weledi na ubunifu ili kuwasaidia wanafunzi kupata maarifa na kufaulu vizuri kwenye mitihani yao,
Aidha amewataka walimu kuzingatia maadili na misingi ya kazi zao kutokana na baadhi ya walimu kujihusisha Kimapenzi na Wanafunzi ili kupunguza vitendo vya ukatili ambavyo vimeendelea kushamiri nchini.
“Natoa onyo kali kwa walimu wachache wenye tabia mbaya zinazochafua sura ya walimu katika jamii, serikali itaendelea kuwashughulikia walimu wenye mwenendo mbaya na kuwachukulia hatua kauli za kisheria,”amesema.
Kwa upande wake Kaimu Rais wa CWT, Dinnah Mathamani, amesema chama hicho kinaridhiwa na uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutatua kero zinazowakabili walimu.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi(CCM), Bara, Christine Mndeme, amewaasa walimu kutokubali kuchonganishwa na kuondolewa umoja wao kwa kuwa ni wazalendo wa kwanza.
Awali akiwasilisha risala ya chama hicho, Kaimu Katibu Mkuu Japhet Maganga, amesema CWT inaomba serikali kuona uwezekano katika bajeti ijayo kutoa nyongeza ya mshahara itakayoendana na gharama halisi ya maisha.
”Nyongeza ya mshahara ya kila mwaka izingatiwe ili kuepuka watumishi kurundikana katika kidato kimoja cha mshahara na hivyo kuwanyima haki wengine kwa kuzingatia umri kazini.”amesema Maganga