Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Benki ya CRDB, Dk Ally Laay (watatu kulia), Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya CRDB, Prof. Neema Mori (wapili kulia), na Mkurugenzi wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (wanne kulia) wakiwa katika kikao na Mkurugenzi wa IFC anayesimamia ushirikiano na Taasisi za Fedha Duniani, Tomasz Telma (wapili kushoto), na Mwakilishi Mkazi wa IFC nchini Tanzania, Frank Ajilore (wakwanza kushoto) walipokutana kujadili ushirikiano baina ya taasisi hizo jijini Washington Marekani jana 14 Desemba 2022. Wengine pichani ni Mkurugenzi wa Mawasiliano Benki ya CRDB, Tully Mwambapa (watatu kushoto), na Mkuu wa Kitengo cha Hazina Benki ya CRDB, Joseph Maji.
Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya CRDB, Prof. Neema Mori (wapili kushoto), na Mkurugenzi wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (wakwanza kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi wa IFC anayesimamia ushirikiano na Taasisi za Fedha Duniani, Tomasz Telma (wapili kulia), na Mwakilishi Mkazi wa IFC nchini Tanzania, Frank Ajilore (wakwanza kushoto) walipokutana kujadili ushirikiano baina ya taasisi hizo jijini Washington Marekani jana 14 Desemba 2022.
—
Washington, Marekani 15 Desemba 2022 – Benki ya CRDB na Shirika la Kimataifa la Fedha la Benki ya Dunia (IFC) wamekubaliana maeneo sita mahususi ya ushirikiano katika juhudi zao za pamoja za kukuza ujumuishi wa kifedha nchini Tanzania na ukanda mzima wa Afrika Mashariki.
Makubaliano hayo yamefikiwa na ndio watendaji wakuu wa taasisi hizo mbili wakati wa mkutano wao huko Washington uluofanyika sambamba na Mkutano wa Wakuu wa nchi za Afrika na Marekani.
Katika mkutano huo, ujumbe wa Benki ya CRDB uliongozwa na Mwenyekiti wa Bodi, Dk Ally Laay, Makamu mwenyekiti, Prof Neema Mori, na Mkurugenzi Mtendaji wa Group, Abdulmajid Nsekela, huku IFC ikiwakilishwa na Mkurugenzi anayesimamia ushirikiano na Taasisi za Fedha Duniani, Tomasz Telma.
IFC ni mshirika wa muda mrefu na wa kimkakati wa Benki ya CRDB na imekuwa na jukumu muhimu katika kusaidia mkakati wa benki tangu 2014.
“IFC imekuwa na mchango mkubwa katika mafanikio ya Benki ya CRDB katika kipindi cha miaka minane iliyopita na katika kufanikisha utekelezaji wa mkakati wetu wa miaka mitano ambao unamalizika mwaka huu,” alisema Nsekela katika taarifa yake iliyowasilishwa kwa vyombo vya habari jijini siku ya Jumatano.
Alisema mkutano wa Washington ulilenga kuwaleta pamoja viongozi wakuu wa taasisi hizo mbili ili kujadili maeneo ya ushirikiano na uungaji mkono.
“Tumekubaliana kushirikiana katika masuala yanayohusu ufadhili wa shughuli za wanawake na vijana; ufadhili wa miundombinu nchini Tanzania, Burundi na DRC, pamoja na kusaidia upanuzi wa huduma za Benki yetu katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini,” Bw Nsekela alisema.
Taasisi hizo mbili, alisema pia zilikubaliana kushirikiana katika ufadhili wa miradi ya mazingira, kilimo biashara, pamoja na kuijengea uwezo Benki ya CRDB katika kubuni na kusimamia miradi ya ufadhili kiuchumi.
Katika maelezo yake wakati wa mkutano huo, Telma alielezea kwa kina uzoefu wa IFC katika kufadhili miradi nchini Tanzania na akabainisha kuwa nchi ina fursa nyingi za kiuchumi, huku akipongeza jitihada zinazofanywa na serikali katika kufungua uchumi.
Alieleza kwa kina uhusiano wa IFC na Benki ya CRDB, na kuipongeza benki hiyo kwa utendaji mzuri kulinganisha na taasisi nyengine za kifedha.
Telma alisema kwa kuwa IFC na Benki ya CRDB wamekuwa wakifanya kazi pamoja kwa miaka mingi, ana matumaini kuwa majadiliano hayo yatafungua fursa mpya za ushirikiano zaidi kati ya taasisi hizo mbili.
Katika mada yake katika mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alieleza kuwa Benki ya CRDB ina mizania ya Sh10.9 trilioni na mtaji wa Sh1.4 trilioni. Benkin hiyo hiyo pia inajivunia kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma za kifedha kupitia njia mbadala na kuchochea ukuaji wa kiuchumi.
Ikiwa na CRDB Wakala zaidi ya 25,000, na huduma mdadala za kidijitali ikiwamo SimBanking, SimAccount, pamoja na ATM za kubadilisha fedha, asilimia 93 ya miamala ya Benki ya CRDB inafanyika nje ya tawi.
Kutokana na ufanisi huo, mwaka 2021 faida halisi ya Benki ya CRDB ilipanda hadi Sh268 bilioni kutoka Sh36 bilioni pekee mwaka 2017 huku faida ya jumla ya miezi tisa ya kwanza ya mwaka huu 2022 wa ikifika Sh257 bilioni.
Benki hiyo imerekodi amana za Sh7.672 trilioni hadi robo ya tatu ya 2022, kutoka Sh4.326 trilioni zilizosajiliwa mwishoni mwa 2017. Vile vile, Benki ya CRDB ilikuwa imefanya uwezeshaji wa mikopo ya jumla ya Sh6.244 hadi kufikia Septemba 30, 2022, kutoka Sh2.894 trilioni mwishoni mwa 2017.
Aidha, Mapato ya Mtaji yameimarika kwa kiasi kikubwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, benki pia imeweza kudhibiti viwango vya Mikopo Chechefu, Uwiano wa Gharama kwa Mapato kufikia viwango vinavyohitajika na Benki Kuu ya Tanzania.
Wakati matayarisho ya utekelezaji wa mkakati wa miaka mitano ijayo (2023 hadi 2027) yakiendelea, Nsekela amesema matarajio ya benki hiyo ni kwamba miaka mitano ijayo itashuhudia kipindi kingine cha ukuaji katika viashiria vyote muhimu vya utendaji.
“Tumetumia miaka 5 iliyopita kuboresha mifumo yetu ya utendaji na utuaji huduma kwa wateja, lakini pia tumejenga msingi sahihi wa kukuza biashara na kuongeza thamani kwa wadau wetu. Mkakati huu mpya unasisitiza katika kuijenga Benki bora zaidi kiutendaji na kuwekeza katika ubunifu wa huduma na bidhaa tukilenga kuboresha maisha ya watu na uchumi kwa ujumla,” alisema.