Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas akizungumzia suala la umuhimu wa mbolea kwenye alipokutana na Kamati ya Ulinzi na Usalama wilaya ya Mbinga katika ziara ya kikazi ya siku moja Baadhi ya wakulima na wananchi mjini Mbinga wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wakati anazungumzia azima ya serikali ya kuhakikisha mbolea ya ruzuku inawafikia wananchi mapema
******************
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amewatoa hofu wananchi kuwa mbolea ipo ya kutosha na kwamba mbolea ndiyo uhai wa Mkoa wa Ruvuma.
Akizungumza na wananchi Wilayani Mbinga Kanali Thomas amesema changamoto ni Mfumo wa kieletroniki ambao unashughuliwa na wananchi watapata mbolea ya ruzuku ambayo imetolewa na Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ili kuwapunguzia gharama kubwa ya mbolea iliyokuwepo Kabla ya Mfumo huu.
Hata hivyo amesema amekutana na Kamati iliyoundwa toka Wizara ya Kilimo ambayo ipo mkoani Ruvuma kwa lengo la kufanya tathmini ya ufuatiliaji wa mbolea ya ruzuku.
“Nawaagiza wakuu wa Wilaya fuatilieni usambazaji wa mbolea na kuhakikisha zinawafikia wananchi,kama kuna mtu yeyote anaficha mbolea achukuliwe hatua “,alisisitiza Kanali Thomas.
Awali akitoa taarifa ya upatikanaji wa mbolea katika Wilaya ya Mbinga,Mkuu wa Wilaya hiyo Mheshimiwa Aziza Mangosongo amesema katika Halmashauri ya Mbinga pekee hadi sasa kuna mbolea zaidi ya tani 2600 na kwamba siku ya Desemba 14 Wilaya imepokea tani 1200 za mbolea ya ruzuku.
Amesema Wilaya inatarajia kutumia vyama vya Ushirika vya Msingi AMCOS kupeleka mbolea kwa wananchi ili kupunguza kero ya umbali.
Mkoa wa Ruvuma kwa miaka minne mfululizo umekuwa ndiyo kapu la chakula la Taifa kwa kuongoza katika uzalishaji wa mazao ya chakula nchini.
Imeandikwa na Albano Midelo wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Mkoa wa Ruvuma
Desemba 15,2022