***********************
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amekabidhiwa Tuzo mbili zilizotolewa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa Kampuni ya DAN AND ASSOCIATES ENTERPRISES LTD (DAE LTD)kutoka Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma .
Akizungumza kabla ya kukabidhi Tuzo hizo kwa Mkuu wa Mkoa katika hafla iliyofanyika kwenye Ofisi za Kampuni hiyo mjini Mbinga,Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya DAN AND ASSOCIATES ENTERPRISES LTD (DAE LTD) Dastan Komba amesema,Kampuni hiyo imekuwa kinara kitaifa wa kupata Tuzo zinazotolewa na Rais katika sekta ya viwanda kwa miaka miwili mfululizo mwaka 2021 na 2022.
“Kampuni ya DAE Ltd imeweza kuwa mshindi bora wa kiwanda cha kati cha uchakataji wa chakula Tanzania (Winner of 2021/2022 Food Processing Medium Scale) kwa miaka miwili mfululizo “,alisema Komba.
Amevitaja vigezo saba vinavyozingatiwa ili kupewa tuzo hizo kuwa ni kiwanda kuzingatia mnyororo mzima wa uchakataji na kiwanda kuzingatia taratibu za ajira na ulipaji mishahara.
Vigezo vingine amevitaja kuwa ni kiwanda kulipa kodi zake zote,matumizi bora ya nishati ya umeme,matumizi ya teknolojia,utunzaji mazingira na matumizi ya vifaa vya kujikinga na Usalama.
Amesema kampuni ya DAE yenye wafanyakazi 150 inamiliki kiwanda cha kahawa,ina miliki hekari 40 zenye miche ya kahawa 20,000 na mitambo 42 ya kuchakata kahawa. Mkurugenzi huyo wa DAE amesema baada ya Rais kumkabidhi Tuzo hizo na yeye ameamua kumkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kwa sababu zimeleta heshima kubwa kwenye Mkoa.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas baada ya kukabidhiwa tuzo hizo amempongeza Mkurugenzi wa DAE kwa kupewa Tuzo mara mbili mfululizo na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Hata hivyo amesema tuzo hizo zimetolewa kwa lengo la kutambua mchango wa Kampuni ya kizalendo katika uzalishaji wa bidhaa za viwandani zenye viwango vya kati.
“Sisi kama Mkoa mafanikio haya tunaona ni fahari kubwa kwetu “,alisisitiza Kanali Thomas.
Licha ya kukabidhiwa tuzo hizo Mkuu wa Mkoa pia alitembelea kiwanda cha Kahawa cha Mwekezaji huyo ambapo ametoa rai kwa wawekezaji wengine kuiga mfano wa kampuni ya DAE LTD iliyofanya uwekaji mkubwa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma Ndugu Oddo Mwisho amesema tuzo hizo zilizotolewa kwa Mwekezaji Mzawa zinadhihirisha kuwa serikali inawajali wawekezaji wa ndani.
Kampuni ya DAE LTD yenye wafanyakazi 150 ilianzishwa mwaka 1988.
Imeandikwa na Albano Midelo wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya MKuu wa Mkoa wa Ruvuma
Desemba 14,2022