Na Mwandishi wetu, Dar es salaam.
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Saalam, imezuia kuendelea mchakato wa mnada wa Kitalu cha uwindaji katika eneo la Jumuiya ya Hifadhi ya Jamii Burunge (JUHIBU)
Mahakama imetoa zuia la dharura la mchakato wa kukigawa kitalu hicho kutokana na kesi iliyofunguliwa na kampuni ya EBN ambayo imekuwa na mkataba katika kitalu hicho tangu mwaka 2013.
Hakimu Mkazi mwandamizi Ferdnadri Kiwonde ametoa uamuzi huo kutokana na maombi ya dharura yaliyowasiloshwa na EBN na kukubaliana na hoja ya msingi kuwa tayari ina mkataba kuendesha kitalu na kutaka kesi ya msingi kusikilizwa.
Zuio la mnada huo liliwekwa na EBN kutokana na maombi namba 176/2023 katika mahakama hiyo ya Kisutu jijini Dar es Salaam kupitia wakili wa EBN Timon Vitalis .
Katika zuio hilo EBN inawafungulia kesi Muungano wa Jumuiya za hifadhi za jamii kwa kutoa Tangazo la zabuni ya Kitalu hicho kinyume cha sheria.
EBN inapinga mchakato wa kukitangaza tena kwa kuwa tayari ilisaini Mkataba mpya tangu Julai 14mwaka huu baada ya tathimini kufanyika iliyohusisha Wizara ya Maliasili na Utalii na taasisi nyingine.
Kesi hiyo inatarajiwa kutajwa januari 14 mwakani na baadae kupangwa siku ya kuanza kusikilizwa.
Wakili Vitalis Akizungumza mwandishi habari hizi Jana alisema baada ya mahakama Kuzuia mnada huo kutokana na maombi yao ya dharura wanatarajiwa kesi ya msingi kupangiwa tarehe ya kutajwa.
Katibu wa JUHIBU WMA Benson Mwaise alikiri jana kupata zuio hilo la mahakama na kueleza kwa Sasa hawezi kulizungumzia.
Mgogoro huo uliibuka katika kitalu hicho kufuatia mwenyekiti wa jumuiya hiyo Juma Hamis kushirikiana na Muungano wa WMA kutangaza upya kitalu hicho licha ya kuwa tayari kuna mkataba umesainiwa.
,Mwenyekiti huyo alikuwa akitaka kampuni nyingine ya uwindaji wa kitalii katika Kitalu hicho na tayari alitoa maamuzi kwa kushirikiana na baadhi ya wajumbe wa baraza la uongoziwa WMA hiyo(AA) kuiondoa bodi ya wadhamini na Katibu wa jumuiya hiyo kwa tuhuma za kusaini mkataba kinyume cha taratibu.
Hata hivyo tayari halmashauri ya Babati imetangaza kuirejesha bodi ya wadhamini na Katibu wa jumuiya hiyo huku ikimsimamisha Mwenyekiti huyo kujihusisha na jumuiya hiyo kupisha ukaguzi wa fedha za jumuiya hiyo.